Na Kassian Nyandindi,
Madaba.
MKUU wa Wilaya ya Songea Mkoani
Ruvuma, Pololet Mgema ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Madaba Mkoani humo
kwa usimamizi na matumizi sahihi ya fedha za Serikali ambazo zinapelekwa katika
Halmashauri hiyo, kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na
kuboresha maisha ya wananchi.
Mgema alitoa kauli hiyo juzi alipotembelea
na kujionea mradi wa ujenzi wa mabweni mawili, madarasa mawili na matundu sita
ya vyoo katika shule ya Sekondari Mahanje iliyopo kata ya Mahanje ndani ya Halmashauri
hiyo ambayo inajengwa kupitia mpango wa P4R.
Serikali imeipatia Halmashauri ya
Madaba, shilingi milioni 196.6 kwa ajili ya kukamilisha kazi hiyo ambapo
mabweni hayo mawili yenye uwezo wa kuchukua watoto 80 kila moja, madarasa na
matundu ya vyoo yamekwisha kamilika.
“Hapa lazima niseme kweli, Mkurugenzi
na uongozi wenu wa shule mmenifurahisha sana na miradi yenu mliyoijenga,
kimsingi imeendana na gharama halisi ya fedha ambazo Serikali ilileta kwa ajili
ya kazi hii, mnastahili pongezi na kuwa mfano wa kuigwa na Wakurugenzi wengine katika
Wilaya yangu”, alisema Mgema.
Vilevile ameutaka uongozi wa shule
hiyo na wanafunzi wake kutunza miradi hiyo ambayo imetumia fedha nyingi za
walipa kodi wa nchi hii, ili iweze kuwa endelevu na itumike kuongeza kiwango
cha taaluma katika shule hiyo.
Alibainisha kuwa Serikali imejenga miundombinu
hiyo kwa lengo la kuboresha mazingira mazuri ya kujifunzia na kufundishia,
hivyo haitakuwa na maana kama kiwango cha ufaulu kitaendelea kushuka.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya
Wilaya Madaba, Shafi Mpenda mbali na kuishukuru Serikali ya awamu ya tano kutoa
fedha hizo kwa ajili ya kuboresha miundombinu hiyo, ameahidi pia kupeleka baadhi
ya vifaa ikiwemo meza na viti kwa ajili ya matumizi ya walimu ili shule iweze
kuendana na ubora wake.
Kwa upande wao nao baadhi ya walimu
wa shule hiyo, wameiomba Serikali kujenga ukumbi wa chakula ili uweze kutumika
kwa ajili ya wanafunzi pale wanapokula chakula.
No comments:
Post a Comment