Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
KUHUSU tatizo la Ukatili wa kijinsia unaofanywa
dhidi ya wanawake, imeelezwa kuwa ni miongoni mwa changamoto kubwa inayoongoza
katika Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma ambapo wanawake wamekuwa wakipigwa,
kubakwa, kutelekezwa na kunyang’anywa mali zao hasa pale waume zao wanapofariki
dunia.
Tatizo hilo hivi sasa limeongezeka na
kukua kwa kasi ambapo katika mwaka 2016 kulikuwa na malalamiko ya ukatili wa
kijinsia 232 ikiwemo miongoni mwao kesi za kubakwa 30 na kupigwa 105.
Imefafanuliwa kuwa wanawake wamekuwa
hawashirikishwi katika kupanga mipango ya miradi ya maendeleo, katika familia
na kupewa fursa ya kufanya maamuzi hivyo kufanya changamoto hiyo kuendelea kuwa
kubwa.
Kufuatia hali hiyo Mkuu wa Mkoa huo,
Christine Mndeme amelitaka Dawati linaloshughulikia masuala ya ukatili wa
kijinsia katika Wilaya ya Mbinga Mkoani humo, kutekeleza majukumu yake ipasavyo
ili kuweza kudhibiti hali hiyo isiweze kuendelea kushamiri miongoni mwa jamii.
Mndeme alisema hayo juzi wakati
alipokuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya siku ya Wanawake duniani,
yaliyofanyika kimkoa katika kijiji cha Lipumba kata ya Kihangimahuka Wilayani hapa.
Alisema kuwa wananchi hususan kundi
la wanawake wanapaswa kwa ujumla wao, kusaidia kutoa taarifa sahihi hasa pale
inapotokea unyanyasaji au ukatili wa aina yoyote ile katika jamii.
“Kuhusiana na masuala ya ukatili wa
kijinsia katika Mkoa huu Mbinga inaongoza, lakini pia hata sisi wazazi
tujitahidi kuwalea watoto wetu wawe na maadili mema, maana jukumu la malezi ya
watoto linaanzia ngazi ya familia tunawajibu kuhakikisha watoto wetu wanapata
mahitaji yao ya msingi bila kuwabagua kwa misingi ya jinsia, ikumbukwe kwamba
kumuelimisha mtoto wa kike ni kueelimisha taifa”, alisema Mndeme.
Alisisitiza kuwa wanawake wanapaswa
kusaidia katika kuhakikisha amani na utulivu, vinakuwepo wakati wote miongoni
mwa jamii na kukemea kwa nguvu zote aina yoyote ile ya ubaguzi pale
unapojitokeza kwani Taifa linataka kuwa na watu wenye maadili mema, uwazi na
uaminifu.
Kwa upande wake, Suzan Hyera ambaye
ni Afisa Mtendaji wa kijiji cha Lipumba Wilayani Mbinga akisoma risala fupi kwa
niaba ya wanawake wa Mkoa wa Ruvuma, mbele ya Mkuu wa Mkoa huo alifafanua kuwa
wanawake wanakabiliwa na changamoto kadha wa kadha ikiwemo vikundi vya wanawake
na vijana, kukosa mikopo au kupewa mikopo kidogo kutoka kwenye taasisi za
kifedha.
Hyera alizitaja changamoto nyingine
kuwa ni wanawake wamekuwa wakitumikishwa katika kazi za kukuza uchumi ambazo
matokeo yake ni kuwafaidisha wanaume, pembejeo za kilimo za ruzuku kutotolewa
kwa wakati na pale zinapotolewa hutolewa kwa kiwango kidogo na kuuzwa kwa bei
juu na kwamba vituo vya kutolea huduma ya afya kukosa waganga wenye sifa na badala
yake wakunga ndio wanakuwa waganga wa vituo.
Alieleza kuwa kumekuwa na upungufu wa
vituo vya kutolea huduma za kiafya katika kata ikiwemo uhaba wa vifaa tiba hasa
kwa akina mama wajawazito na watoto, kwani hilo limekuwa ni tatizo katika Mkoa wa
Ruvuma hasa kwa maeneo ya vijijini wamekuwa wakikosa hata miundombinu imara na
salama ya maji ya bomba.
Pia aliongeza kuwa ili waweze kuwa na
afya bora katika kuinua uchumi wa familia pamoja na Taifa kwa ujumla na kuweza
kufikia kauli mbiu ya siku ya maadhimisho ya wanawake duniani isemayo; “Kuelekea uchumi wa viwanda tuimarishe
usawa wa jinsia na uwekezaji wa wananchi vijijini” ni lazima sasa viongozi
ndani ya Halmashauri za Wilaya wajitahidi kutunisha mfuko wa wanawake na vijana
ili walengwa waendelee kupata mikopo yenye riba nafuu.
No comments:
Post a Comment