Na Yeremias Ngerangera,
Namtumbo.
HALMASHAURI ya Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma, imetumia
kiasi cha shilingi Bilioni 3.6 kuwawezesha wanufaika wa kaya maskini tangu mpango
huo, ulipoanzishwa Wilayani humo mwaka 2015.
Raphael Mponda ambaye ndiye Mratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya
Jamii (TASAF) Wilayani hapa, alisema hayo juzi wakati alipokuwa akizungumza na
mwandishi wa habari hizi mjini hapa.
Alisema kuwa wameweza kuwalipa wanufaika hao kwa awamu 16 Wilayani
Namtumbo tangu mpango huo uanzishwe.
Mponda alieleza kuwa mafanikio ya mpango huo kwa wanufaika wa
kaya maskini kuwa ni pamoja na kaya 2,073 kati ya kaya 5,559 ambazo zimejiunga
na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).
Kufuatia utekelezaji huo mahudhurio ya watoto shuleni
yameongezeka na kwamba kaya zinazonufaika zimeweza kuboresha pia makazi yao na
watoto 181 waliopo kwenye kaya hizo wamehitimu darasa la saba mwaka 2017 na
kuweza kujiunga kidato cha kwanza mwaka huu.
Baadhi ya wanufaika wa kaya maskini, Zena Faraji kutoka kijiji
cha Suluti na Ridhiki Issa wa kijiji cha Nahoro walidai kuwa mpango wa kunusuru
kaya maskini, umeboresha maisha yao kutokana na kujikita zaidi katika shughuli
za kilimo na kufuga mifugo iliyonunuliwa na fedha zinazotolewa na Serikali.
Wanufaika hao walidai kuwa wamejiunga katika vikundi vya kaya
maskini vya kuweka na kukopa, ambavyo vinawawezesha kuweka fedha zao na kukopa
fedha kwa ajili ya kufanya biashara ndogo ndogo.
Naye Kaimu Ofisa maendeleo ya jamii, Owigo Phinias pamoja na
mambo mengine alisema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo ina vikundi 28 vya
wanufaika wa kaya maskini ambapo baadhi ya vikundi vimefikia hatua ya kupata usajili
baada ya kutimiza masharti husika, huku baadhi ya vikundi vingine vikiendelea
na hatua ya usajili kwa lengo la kuwawezesha kukopa fedha katika mfuko wa
wanawake unaotolewa na Halmashauri hiyo.
No comments:
Post a Comment