Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
JUMUIYA ya Umoja wa Wanawake Tanzania
(UWT) imesema kuwa wanataka kuona kwamba inakuwa kimbilio kubwa kwa Wanawake,
katika kuanzisha vikundi vya ujasiriamali ambavyo vitaweza kuwakomboa waweze
kuondokana na umaskini.
Vikundi hivyo imesisitizwa kuwa
viundwe na kusajiliwa kisheria ili kuweza kukuza uchumi wa akina mama na kujenga
mshikamano wa pamoja utakaowafanya waache tabia ya kuwa na makundi ambayo hapo
baadaye yanawagawa wao na chama kwa ujumla.
Amina Makillagi ambaye ni Katibu Mkuu
wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) alisema hayo juzi, alipokuwa katika ziara
yake ya siku mbili Wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma akitembelea kujionea
maendeleo ya umoja huo.
Alisema kuwa hizi ni zama za ukweli
na uwazi ambapo viongozi umefika wakati sasa wa kusimamia maadili mema ya
mwanachama ili waweze kuepukana na matendo yanayorudisha nyuma maendeleo yao.
Pia alisisitiza kuwa katika vikundi
hivyo wanapaswa wajishughulishe na shughuli za ufugaji wa mifugo ya aina
mbalimbali, kilimo na biashara ndogo ndogo ambavyo vitaweza kuwaingizia kipato
na kusukuma mbele maisha yao.
No comments:
Post a Comment