Na Kassian Nyandindi,
Songea.
Songea.
WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA)
wamekabidhi jengo moja, ambalo ni bweni la kulala wanafunzi katika shule ya Sekondari
ya Wasichana Songea iliyopo Mkoani Ruvuma, ambalo limekarabatiwa kwa zaidi ya shilingi
Milioni 102.
Kabla ya kukabidhi jengo hilo umefanyika
ukaguzi wa bweni hilo ambalo ni la ghorofa likiwa na uwezo wa kuchukua Wanafunzi
110.
Ukaguzi huo uliwashirikisha watalaamu
kutoka Manispaa ya Songea wakiwemo na mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa hiyo
Frowin Komba, Mhandisi wa ujenzi Karoline Kandonga, Mkuu wa shule hiyo Tupoke Ngwala,
Mwakilishi wa TBA Mhandisi Eugenics Thomas na viongozi wa Serikali ya wanafunzi
katika shule ya Sekondari ya Wasichana Songea.
Akizungumza juzi baada ya kukabidhi
mradi huo mwakilishi wa TBA Mhandisi Eugenics Thomas alisema kuwa ukarabati wa
bweni hilo ulianza Januari 10 mwaka huu na kwamba, ukarabati wa mabweni mengine
matano unaendelea kufanywa shuleni hapo kwa awamu ambapo ukarabati wa bweni la
pili utaanza rasmi mwezi Aprili mwaka huu.
Vilevile alitoa rai kwa wanafunzi wa
shule hiyo ya Sekondari ambao wataingia katika bweni hilo lenye vitanda 110 na
makabati 110 kuhakikisha kwamba wanatunza bweni hilo liwe wakati wote katika
hali nzuri ya usafi kwa kuwa Serikali imetumia fedha nyingi za kukarabati.
Kwa upande wake Mkuu wa shule ya
Sekondari ya Wasichana Songea, Tupoke Ngwala alisema Serikali imetoa zaidi ya
shilingi bilioni 1.6 kwa ajili ya kufanyia ukarabati majengo yote ya shule hiyo,
yakiwemo mabweni na majengo ya utawala.
Shule ya Sekondari ya Wasichana
Songea ni miongoni mwa shule kongwe hapa nchini, ina wanafunzi 874 wanaosoma
kidato cha tano na sita ambayo ilianzishwa mwaka 1974.
No comments:
Post a Comment