Na Mwandishi wetu,
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa
amewataka Mawaziri wa Afya kutoka nchi tisa za Afrika kutoa mapendekezo ya namna
ya kutokomeza magonjwa yasiyo ambukiza, kwa wakuu wa nchi hizo ili yafanyiwe
kazi haraka.
Aliyasema hayo jana Machi 19 mwaka
huu wakati alipokuwa akifungua Mkutano wa 65 wa Mawaziri wa Afya, kutoka nchi
tisa wanachama wa Jumuiya ya Afya kwa nchi za Afrika Mashariki, Kati na
Kusini (ECSA-HC).
Alisema kuwa magonjwa yasiyo ambukiza
ni miongoni mwa magonjwa ambayo yameendelea kuwatesa wananchi kwa kiasi kikubwa,
katika nchi nyingi za Bara la Afrika hivyo vyema mawaziri hao wakatoa mapendekezo
ya namna ya kuyatokomeza.
Waziri Mkuu alifafanua kuwa magonjwa
hayo, yanaweza kudhibitiwa kwa kuhamasisha wananchi kuboresha lishe na
kusisitiza ulaji wa vyakula bora, kufanya mazoezi na kubadili mitindo ya
maisha.
“Magonjwa yasiyoambukiza yanaongoza
kwa kusababisha vifo katika baadhi ya nchi wanachama wa ECSA. Magonjwa haya
yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya mfumo wetu wa lishe na maisha,
hivyo ni muhimu suala hili likatafutiwa ufumbuzi”, alisema Majaliwa.
Waziri Mkuu huyo alieleza kuwa magonjwa
yasiyoambukiza pamoja na magonjwa mengine ya milipuko kama vile ebola, homa ya
bonde la ufa, dengue, homa ya manjano yamekuwa kikwazo cha maendeleo kwa katika
baadhi ya nchi.
Pia aliongeza kuwa sekta ya afya ni
muhimu kwa ajili ya kuboresha maendeleo ya nchi zote ikiwemo zilizoendelea na
zinazoendelea, hivyo changamoto zote zinazoikabili zinapaswa kupewa kipaumbele
katika utatuzi huo.
Kwa upande wake Waziri wa Afya,
Jinsia, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema malengo ya
mkutano huo ni kuzungumzia changamoto mbalimbali zinazohusu sekta ya Afya na
kuyapatia ufumbuzi.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Mawaziri
wa Afya kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afya kwa nchi za Afrika Mashariki,
Kati na Kusini ambazo ni Tanzania, Malawi, Lesotho, Uganda, Kenya, Rwanda,
Zambia, Zimbabwe na Muwakilishi kutoka nchini Mauritius.
Pia Katibu wa jumuiya hiyo Profesa
Yoswa Dambisya, Muwakilishi wa Benki ya Dunia Dokta Paolo Belli pamoja na wadau
wa sekta ya afya kutoka nchi hizo.
No comments:
Post a Comment