Na Muhidin Amri,
Tunduru.
VIONGOZI na Wanachama 1,630 wa Chama
cha ACT– Wazalendo katika Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma, wamefunga milango ya
chama chao na kukihama chama hicho huku wakijiunga na Chama Cha Mapinduzi
(CCM).
Wanachama hao walifikia maamuzi hayo
juzi mbele ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Rodrick Mpogoro katika kijiji cha
Mtina Wilayani Tunduru Mkoani hapa kwa kile walichodai kwamba wanaunga mkono
juhudi za Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dokta John Pombe Magufuli
ambaye amekuwa akionesha kupambana kwa vitendo hasa katika matukio ya ufisadi, rushwa
wizi na dhuluma.
Akizungumza kwa niaba ya Wanachama
wenzake Afisa wa ACT, Amani Ramadhan Kawawa alisema kuwa yeye na wanachama
wenzake katika Wilaya hiyo wamefikia maamuzi hayo, baada ya kubaini kuwa
viongozi wa vyama vya upinzani wamekuwa wakiwatumia wao kama daraja la kuweza
kufikia mafanikio yao binafsi.
Kawawa alisema kuwa kutokana na
maamuzi hayo, amejiudhuru nafasi zake zote alizokuwa anaziongoza kupitia chama
hicho cha ACT.
Alisema mbali na viongozi hao wa
vyama vya siasa kuahidi kufikia malengo ya kuchukua dola, lakini hali halisi ya
utekelezaji wa malengo hayo umekuwa hauendani na utekelezaji wake jambo ambalo
linawafanya wajitambue na kuwaona kuwa viongozi hao ni matapeli.
Alisema kuwa chama chochote ambacho
kinahitaji kuchukua dola kinatakiwa kuwa karibu na jamii, lakini vyama vingi vya
siasa hapa nchini kwa muda mrefu havijaonesha kuwa na mahusiano ya karibu na
wanachama wake hasa katika kushiriki shughuli za kimaendeleo, badala yake
vimekuwa vikitumia muda mwingi kuchochea chuki na uhasama kati ya wananchi na Serikali
yao.
Kawawa aliwataja viongozi wengine
ambao wameunga mkono maamuzi hayo kuwa ni pamoja na Mohamed Kisonga Zuberi
(Mwenyekiti na mgombea udiwani kata ya Nampungu), Rashid Hashim Mbalamula (Katibu
Mwenezi Act – Wilaya) Wenyeviti, Makatibu kata zote Wilayani humo pamoja na wanachama
katika vijiji vyote vya Wilaya hiyo.
Mbali na Kawawa, Wanachama wengine wa
ACT waliojiunga na Chama Cha Mapinduzi ni pamoja na Alli Daimu Abdalah ambaye
alikuwa Mwenyekiti wa ACT – Wazalendo na mgombea Ubunge katika jimbo la Tunduru
Kusini katika uchaguzo Mkuu uliopita wa mwaka 2015.
Akiwakaribisha wanachama hao Naibu
Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Mpogolo pamoja na kuwapongeza kwa maamuzi hayo
waliyofanya aliwataka Watanzania, ambao bado wapo katika vyama vya upinzani kurudi
katika Chama Cha Mapinduzi ambacho kimepigania Uhuru wa nchi hii.
Mpogolo alieleza kuwa utekelezaji wa
Serikali ya awamu ya tano inashughulika na kero za wananchi wake kwa kasi ya
ajabu na kuwaletea maendeleo hivyo haoni sababu ya wao kupoteza muda na
kuhangaika na vyama vyenye ukakasi.
Aliongeza kuwa hivi sasa Tunduru
imefunguka kwa kuwa na miundombinu mizuri na yenye uhakika ya barabara,
mawasiliano, nishati ya umeme, maji na afya.
No comments:
Post a Comment