Na Kassian Nyandindi,
Songea.
MAFUNZO ya utoaji wa Chanjo ya Saratani
mlango wa kizazi, kwa wasichana wenye umri kuanzia miaka tisa hadi 14 yamefanyika
katika Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma.
Aidha mafunzo hayo yameshirikisha Walimu
wa afya kutoka shule za Msingi na Sekondari na Wahudumu wa afya ya msingi zaidi
ya 300 kutoka katika Manispaa hiyo mjini hapa.
Kufanyika kwa zoezi hilo kunalenga
kwamba kabla ya siku ya Jumatatu Aprili 23 mwaka huu, siku hiyo utafanyika
uzinduzi wa Mkoa huo wa chanjo hiyo kwa wasichana wenye umri huo.
Uzinduzi huo kimkoa unatarajiwa kufanywa
na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christine Mndeme.
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa huo, Dokta
Mameritha Basike alisema hayo leo wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo kwa niaba
ya Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Songea, Tina Sekambo.
Dokta Basike amelitaja lengo la
Manispaa hiyo ni kutoa chanjo ya Saratani mlango wa kizazi kwa wasichana 1,834
na kwamba lengo la Mkoa ni kutoa chanjo hiyo kwa wasichana 28,676.
“Manispaa ya Songea tumejipanga
kuhakikisha kuwa tunatoa chanjo hii kwa asilimia kati ya 99 hadi 100, zoezi hili
katika Mkoa wetu litaanza Aprili 23 hadi 29 baada ya hapo zoezi hili la utoaji
chanjo ya Saratani mlango wa kizazi litakuwa endelevu”, alisema Dokta Basike.
Alisema kuwa chanjo hiyo ni muhimu kwa
sababu itapambana na Virusi vinavyoitwa Human Papiloma Virus (HPV) ambavyo huambukizwa
kwa njia ya ngono na kwamba chanjo inakusudia kuweka kinga dhidi ya kirusi hicho
ambacho kinasababishwa na kufanya ngono hasa katika umri mdogo.
Mmoja wa watoa mada katika mafunzo hayo,
Flowin Komba amevitaja visababishi vya Saratani hiyo ni kuanza ngono katika umri
mdogo, kufanya ngono na wapenzi wengi, historia ya kubeba mimba nyingi na uvutaji
wa sigara, tumbaku na ugoro.
Takwimu zinaonesha kuwa kila mwaka wagonjwa
6,000 wa Saratani mlango wa kizazi na matiti wanagundulika kuwa na magonjwa
hayo huku kati yao wagonjwa 4,000 hupoteza maisha.
Takwimu kutoka Taasisi ya Saratani ya
Ocean Road iliyopo Jijini Dar es Salaam, inaonesha kwamba mwaka 2015 Tanzania
ilikuwa na wagonjwa wa Saratani 2,500 ambapo mwaka huo idadi hiyo, iliongezeka hadi
kufikia 5,200 sawa na ongezeko la asilimia 100.
Kulingana na takwimu hizo Saratani ya
mlango wa kizazi na matiti husababisha asilimia 50 ya vifo, vinavyotokana na Saratani
kwa akina mama na kwamba kila watu 100 wanaochunguzwa hubainika wagonjwa 36
kuwa na Saratani.
No comments:
Post a Comment