Wednesday, April 4, 2018

TFS YAPANDA MITI HEKTA 1,630 MADABA WANANCHI WAPEWA MICHE BURE


Na Muhidin Amri,   
Madaba.

WAKALA wa Huduma za Misitu Nchini (TFS) kupitia shamba la miti Wino lililopo katika kata ya Wino Halmashauri ya Wilaya ya Madaba Mkoani Ruvuma, kwa muda wa miaka miwili kuanzia mwaka 2016 hadi 2017 Wakala huyo ameweza kupanda hekta 1,630 za miti ya aina mbalimbali.

Mbali na kupanda idadi ya miti hiyo, amefanikiwa kutoa miche ya miti bure kwa wananchi na vikundi vilivyoamua kuanzisha mashamba ya miti kibiashara, ili waweze kujikwamua na umaskini baada ya kuonekana kwamba zao la miti lina soko kubwa hapa nchini.

Kaimu Meneja wa shamba hilo, Haji Mpya alisema hayo juzi wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi katika kijiji cha Wino, Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.


Alisema kuwa mbali na kupanda na kugawa miti, pia wamekuwa wakitoa elimu kwa wananchi wa vijiji jirani na shamba hilo namna ya kupata mbegu bora na kuanzisha bustani zao za miche, kuandaa mashamba, kupanda, kuitunza, kuzuia na kuzima moto katika mashamba ya miti hasa kipindi cha kiangazi.

Alieleza kuwa shamba la Wino ambalo lina ukubwa wa hekta 17,000 ambapo eneo hilo lote la shamba la miti, limeshapandwa na sasa shughuli zinazoendelea ni utunzaji wa miti kama vile kupalilia na ulinzi kwa ajili ya kuzuia kutokea majanga ya moto.

Vilevile kazi ya upandaji miti imekuwa ikiendelea kufanyika katika mashamba mengine ya Ifinga na Mkongotema kwani eneo la Wino limeshajaa.

Katika kipindi cha miaka miwili ya utawala wa Rais Dokta John Magufuri, shamba la miti Wino limechangia jumla ya Shilingi milioni 26.234 katika kufanikisha kuandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi katika vijiji vya Mkongotema na Ifinga.

Haji aliongeza kuwa katika kipindi hicho wamechangia mradi mkubwa wa usambaji maji katika kijiji cha Ifinga, kwa kununua vifaa vya usambaji maji vyenye thamani ya Shilingi milioni 37.266 ambavyo vimekabidhiwa kwa uongozi wa kijiji hicho.

Mbali na fedha hizo, TFS kupitia mradi wake wa shamba la miti Wino wamekubali kugharamia mradi mpya wa maji ya mtiririko katika kijiji cha Ifinga ili kuweza kuwaondolea kero ya maji wananchi wa kijiji hicho.

Hata hivyo Wakala huyo wa huduma za misitu ni taasisi endelevu ambayo itaendelea kusimamia utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) chini ya Serikali ya Rais Dokta John Magufuli kwa mujibu wa sera, sheria, kanuni na miongozo mbalimbali ya Serikali kwa lengo la kulinda rasilimali za misitu na kuboresha mazingira.

No comments: