Machinjio ya Halmashauri ya Mji wa Mbinga Mkoani Ruvuma, ambayo inalalamikiwa kukosa huduma ya maji na kushamiri kwa uchafu. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WACHINJAJI wa ng’ombe katika
Halmashauri ya Mji wa Mbinga Mkoani Ruvuma, wamesema kwamba wanashindwa kufanya
kazi ya uchinjaji ng’ombe katika machinjio ya Halmashauri hiyo, iliyopo mjini
hapa kutokana na kukosa huduma ya maji.
Aidha kufuatia uwepo wa tatizo la
ukosefu wa huduma hiyo muhimu machinjio hiyo imekuwa katika hali mbaya kutokana
na kukithiri kwa uchafu.
Wauzaji wa nyama ya ng’ombe mjini
hapa nao jana wametia mgomo wa muda usiojulikana wakikataa kutoa huduma ya
uchinjaji na uuzaji nyama, mpaka Mamlaka husika itakapoweza kutatua tatizo hilo
ambalo limedumu kwa muda mrefu na kuwa kero kubwa.
Simon Mbunda ambaye ni mhudumu wa
kufanya usafi katika machinjio hiyo aliwaeleza Waandishi wa habari kuwa,
amekuwa akishindwa wakati mwingine kufanya usafi katika eneo hilo kutokana na
kukosa vitendea kazi husika kama vile buti za kuvaa miguuni mwake.
Naye Mkaguzi wa nyama katika
Halmashauri ya Mji wa Mbinga, Geofrey Noel alisema kuwa wamezuia uchinjaji huo
kuanzia Aprili 19 mwaka huu mpaka waweze kuwa na uhakika wa kupata huduma hiyo ya
maji.
Alieleza kuwa tatizo kubwa la ukosefu
wa maji kwenye machinjio hiyo linatokana na mfumo uliojengwa na Mamlaka ya Maji
safi na Usafi wa Mazingira Mji wa Mbinga (MBIUWASA) kutoleta maji ipasavyo
katika matenki yaliyojengwa katika eneo hilo.
Noel alibainisha kuwa hata mafundi wa
Mamlaka hiyo ya maji licha ya kupewa taarifa miezi kadhaa iliyopita juu ya hali
hiyo, lakini wamekuwa wazembe kufanya ufuatiliaji na matengenezo madogo katika mfumo
huo.
“Mafundi hawa wamekuwa hawafiki hapa
mara kwa mara kufanya matengenezo madogo madogo pale tatizo linapojitokeza,
wanakuja wanapotaka wao na tatizo la ukosefu wa maji katika machinjio hii lina
muda mrefu sasa hakuna utekelezaji unaofanyika”, alisema Noel.
Naye Mwenyekiti wa Wachinjaji ng’ombe
katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga, Joseph Chawala alisema kuwa licha ya
kupeleka malalamiko yao mara kwa mara kwa uongozi wa Halmashauri ya Mji huo akishirikiana
na Daktari wa mifugo wa Mji, hakuna utekelezaji uliofanyika kwa muda mrefu
sasa.
Chawala alisema kuwa kwa siku za
nyuma wamekuwa wakilazimika kuomba maji ya kisima nyumba jirani iliyopo karibu na
machinjio hayo, jambo ambalo wamefikia hatua ya kuchoka na kuitaka Halmashauri
itatue haraka tatizo hilo, kwani wamekuwa wakikusanya ushuru kupitia uchinjaji pale
unapofanyika.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji
wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga, Robert Mageni alipotafutwa ili aweze kutolea
ufafanuzi juu ya changamoto hizo hakuweza kupatikana Ofisini kwake.
No comments:
Post a Comment