Na Muhidin Amri,
Tunduru.
WANANCHI wa Kijiji cha Tuwemacho kata
ya Tuwemacho Wilaya ya Tunduru Mkoa wa Ruvuma kwa kushirikiana na Mfuko wa Maendeleo
ya Jamii (TASAF) hapa nchini, wamefanikiwa kujenga bwawa kubwa la maji safi ili
kuweza kumaliza kero ya muda mrefu ya upatikanaji wa huduma ya maji
safi na salama.
Kuchimbwa kwa bwawa hilo, kumekuja
baada ya vyanzo vya maji vilivyopo kwenye kijiji hicho kushindwa kukidhi
mahitaji halisi ya wananchi husika, kutokana na ongezeko kubwa la wageni
wanaofika kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo cha zao maarufu la
korosho.
Afisa Mtendaji wa kijiji cha
Tuwemacho, Ali Fadhil alisema kuwa TASAF kupitia mpango wa kunusuru kaya
maskini katika kijiji hicho, umewezesha kupatikana kwa majawabu mengi ya kero za
wananchi ikiwemo ukosefu wa huduma ya maji.
“Tulikuwa na tatizo kubwa la
upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, lakini kupitia miradi shirikishi
tuliamua kuboresha visima vya asili vya maji pamoja na kuhifadhi vyanzo vya
maji kwa kupanda miti ambayo ni rafiki ya maji”, alisema Fadhil.
Katika mkutano uliofanyika kijijini
hapo, kwa nyakati tofauti ilielezwa kuwa hali ya upatikanaji wa maji bado
imekuwa ni tatizo kwa wananchi hao hivyo kuna kila sababu ya kuendelea
kutengeneza ubunifu wa vyanzo vipya vya maji, ambavyo vitaweza kuendelea
kusaidia wananchi katika maisha yao ya kila siku.
Wananchi walisema katika mkutano huo kwamba
wamekubaliana kuchangia kiasi cha shilingi 2,500 kwa kila kaya ikiwa
ni hatua ya kuanzisha ujenzi wa miundombinu ya maji na fedha
zilizokusanywa hadi kufikia Machi 20 mwaka huu zimefikia Shilingi milioni
1,500,000.
Fedha hizo imeelezwa kuwa zitatumika
kununulia vifaa kama vile mabomba pamoja na pampu za kusukumia maji kutoka
kwenye chanzo na kwamba michango hiyo bado inaendelea kuchangishwa ili kuweza
kupata fedha zitakazotosheleza kutekeleza mradi huo wa maji.
No comments:
Post a Comment