Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
UKOSEFU wa gari maalum la kusambazia
chanjo na vifaa tiba vya kutolea huduma, imeelezwa kuwa ni changamoto kubwa
inayoikabili idara ya afya kitengo cha huduma ya afya ya uzazi na mtoto katika vituo
vya afya, vilivyopo Halmashauri ya Mji wa Mbinga Mkoani Ruvuma.
Kufuatia uwepo wa tatizo hilo,
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya afya Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeombwa kumaliza kero hiyo ndani ya Halmashauri
hiyo ili kuweza kuleta ufanisi mzuri wa utendaji kazi kwa idara hiyo katika
jamii.
Hayo yalisemwa na Muuguzi wa afya Hospitali
ya Halmashauri ya Mji Mbinga, Verena Mapunda alipokuwa akisoma risala ya
uzinduzi wa wiki ya chanjo duniani kwa Halmashauri ya Mji huo uliofanyika mjini
hapa.
Uzinduzi huo ulifanywa na Mkuu wa
Wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye ambapo katika kuadhimisha wiki hiyo kutakuwa
na uanzishwaji wa chanjo ya kuzuia Saratani ya mlango wa shingo ya kizazi kwa
wasichana wenye umri wa miaka 9 hadi 14 (Human Papiloma Virus) ambayo itatolewa
sambamba na chanjo nyingingine ya ziada inayokinga ugonjwa wa Polio.
Mapunda alifafanua kuwa zoezi hilo
linalenga pia utoaji wa elimu endelevu kwa jamii ili iweze kutambua umuhimu wa
chanjo kwa watoto wao na kuweza kuhamasika kushiriki kikamilifu katika
kuhakikisha kwamba wanapata chanjo kwa wakati kulingana na ratiba iliyopangwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo,
Nshenye alisisitiza kuwa katika kuzingatia kauli mbiu ya siku ya chanjo duniani
isemayo, Jamii iliyopata chanjo ni jamii yenye afya timiza wajibu wako,
wananchi sasa wanapaswa kujitokeza kwa wingi kushiriki kikamilifu katika zoezi
hilo ili kuwezesha kuwa na jamii imara na madhubuti kiafya ambayo haishambuliwi
na magonjwa kwa urahisi.
Pia Nshenye amewataka viongozi wa Mji
huo kuhimiza jamii kwa kutoa elimu endelevu kuhusu chanjo hiyo ili wazazi
waweze kupeleka watoto wao katika vituo vya kutolea huduma ya afya.
Hata hivyo Mji wa Mbinga katika
utekelezaji wa zoezi hili wanatarajia kuwafikia watoto 1,326 kwa wale wasiopata
chanjo, ili waweze kupewa huduma husika na hatimaye waepukane na magonjwa
yanayoweza kuathiri afya zao hapo baadaye.
No comments:
Post a Comment