Na Kassian Nyandindi,
Songea.
BAADHI ya Wakulima wanaozalisha zao
la kahawa katika Wilaya ya Songea, Mbinga na Nyasa Mkoani Ruvuma wameitaka Bodi
ya Kahawa Tanzania (TCB) kuwawezesha kujisajili kwenye mfumo wa utoaji wa
taarifa za masoko ya dunia, ili mauzo ya kahawa yao yaendane na soko hilo.
Pia walisema kuwa ili waweze kuuza
kahawa yao moja kwa moja mnadani bila kupitia kwa mtu binafsi ni muhimu waingizwe
kwenye mfumo huo ili watambue soko la dunia lipoje.
Walisema hayo kwa nyakati tofauti
Mkoani humo wakati walipokuwa wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa
sharti la kutotajwa majina yao gazetini.
Walisema kuwa kwa kufanya hivyo
kutawafanya wakulima wa kahawa kuepukana na wafanyabiashara wajanja ambao
huwatapeli fedha zao kupitia mauzo ya kahawa yao mnadani.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya
kahawa Tanzania, Primus Kimaryo alipohojiwa alisema kuwa bodi hiyo inao uwezo
wa kusimamia hilo na wakulima wataweza kuingizwa kwenye mfumo wa kupata taarifa
za soko la dunia kwa wakati.
Alisema kuwa namna ya kuweza
kujisajili na mfumo huo ni gharama ya dola za Kimarekani 1,000 na kwamba
kupitia kwenye vyama vyao vya ushirika wataweza kuanza kuwasajili kuanzia
mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu.
“Masoko yatakapofunguliwa na minada
ya kahawa kuanza ndipo bodi inatarajia kuanza kazi hii ya kusajili wakulima
mfumo wa utoaji taarifa za masoko ya dunia ili mauzo ya kahawa zao ziendane na
soko hilo”, alisema Kimaryo.
Vilevile Meneja wa Kiwanda cha
Kukoboa Kahawa Wilayani Mbinga (MCCCO), Jonas Mbunda amenukuliwa na vyombo vya
habari akiiomba Serikali kuweka sera itakayosaidia kuongeza uzalishaji wa zao
la kahawa kwa wakulima pamoja na uhamasishaji unywaji wa kahawa ya ndani ya
nchi.
Alisema Serikali inatakiwa
kuhakikisha kwamba inatafuta masoko ya uhakika kwa ajili ya kuwafanya wakulima
hao waweze kuuza kahawa yao kwa bei nzuri.
Mbunda alifafanua kuwa endapo
itasimamia mambo hayo kikamilifu maendeleo ya uzalishaji wa zao la kahawa Mkoani
Ruvuma katika Wilaya hizo yatakuwa juu na hatimaye kuweza kufikia malengo husika.
Alibainisha kuwa MCCCO mkakati
walionao hivi sasa katika kujiongezea mapato ni kuendelea kutoa huduma bora kwa
wateja wake ili kuweza kupata kiasi kikubwa cha kahawa kinachozidi asilimia 60
ambazo wanazipata hivi sasa.
Kadhalika mkakati mwingine walionao aliongeza
kuwa watajenga kiwanda kidogo cha kusindika kahawa ya kunywa ambayo huyeyuka
mara moja pamoja na kuendelea na biashara ya ununuzi wa kahawa bora.
“Kiwanda hiki cha kukoboa kahawa hapa
Mbinga kinao uwezo wa kukoboa tani 12 za kahawa kwa saa na tani 30,000 katika
msimu kwa mwaka, lakini tukiangalia kwenye orodha ya mapokezi wakati kiwanda
kimeanza 1989 hadi sasa 2018,
“Hakuna uwezo wa kupokea kahawa zaidi
ya tani 10,000 tumekuwa tukipokea tani 5,000 hadi 10,000 maana yake ni kwamba
kinafanya kazi chini ya uwezo wake kutokana na uzalishaji wa kahawa hapa Mbinga
kuwa kidogo”, alisema Mbunda.
Meneja huyo alisema kuwa hali ya
uchumi wa kiwanda hicho kutoka mwaka 2012 hadi 2017 kinaendeshwa kwa faida na
kwamba hakijawahi kupata hasara katika kipindi hicho cha miaka mitano na kwamba
kimekuwa kikilipa kodi zote za Serikali na kimeweza kupata hati tuzo ya kuwa
mlipa kodi mkubwa katika ngazi ya Wilaya kwa kipindi cha miaka minne mfululizo.
Pamoja na mambo mengine Kiwanda cha
kukoboa kahawa Wilayani Mbinga kinamilikiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania kwa asilimia 43 na asilimia 57 kutoka kwenye vyama vya ushirika
vinavyolima zao la kahawa hapa nchini.
No comments:
Post a Comment