Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Cosmas Nshenye
amewataka watendaji waliopo katika halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani humo kuhakikisha
kwamba wanatekeleza kwa haraka zoezi la ujenzi wa vyoo bora mashuleni, ili
wanafunzi waweze kuepukana na magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu.
Zoezi hilo la ujenzi wa vyoo hivyo alisema kuwa anataka
lianze mara moja kuanzia sasa, kwa shule za msingi na sekondari ambazo kuna
tatizo la upungufu wa vyoo ili kuweza kuepukana na watoto kujisaidia vichakani.
Agizo hilo la Mkuu huyo wa wilaya lilitolewa juzi kwenye
kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya mji huo, kilichofanyika mjini
hapa katika ukumbi wa Jumba la maendeleo.
“Suala la ujenzi wa vyoo ni lazima litekelezwe kuanzia sasa,
nataka mikakati ya kuhakikisha kwamba kila shule ya msingi na sekondari
inatekeleza jambo hili mapema na kwa kasi kubwa”, alisisitiza Nshenye.
Alibainisha kuwa yeye hapendi kusikia wataalamu katika wilaya
hiyo wanavutana bali anatarajia kusikia wanapigania maendeleo ya wananchi kwa
faida ya kizazi cha sasa baadaye.
Nshenye alisema kuwa kama wataishia kulumbana maana yake
hawataweza kufikia malengo husika ya kuhudumia wananchi, hivyo amewataka
wafanye kazi kwa kujituma na sio muda mwingi kukaa maofisini.
“Ndugu zangu mtumishi yeyote aliyeajiriwa na serikali
asitafute utajiri kwenye makaratasi, nikisema hivi najua mnanielewa yatupasa
tukubali kwamba ulikubali kuajiriwa kwa ajili ya kuwatumikia wananchi”,
alisema.
No comments:
Post a Comment