Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WAUGUZI wa idara ya afya, hospitali ya Halmashauri ya mji wa
Mbinga mkoani Ruvuma wameulalamikia uongozi wa Chama cha akiba na mikopo,
Kurugenzi SACCOS kilichopo mjini hapa kwa kushindwa kuwalipa madai yao ya fedha
kwa miaka mingi huku wakieleza kuwa, watakwenda kuushtaki uongozi husika
Mahakamani ili waweze kupata fedha zao.
Aidha walisema kuwa madai wanayodai ni yale ambayo yanatokana
na makato mbalimbali wanayokatwa katika mishahara yao, hivyo hawaoni sababu ya
kuendelea kuwa wanachama katika SACCOS hiyo kutokana na manyanyaso
wanayoyapata.
Hayo yalisemwa na Wauguzi hao walipokuwa wakizungumza na
Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini, Sixtus Mapunda katika kikao maalum kilichoketi
jana katika jengo la hospitali hiyo mjini hapa.
Walisema kuwa licha ya suala hilo kufikishwa katika ngazi
mbalimbali ya ofisi za serikali, utekelezaji wake umekuwa hauzai matunda na
kwamba walimuomba Mbunge huyo aingilie kati ili waweze kupata haki zao za
msingi.
Kwa upande wake Mbunge Mapunda alipokuwa akitolea ufafanuzi
juu ya malalamiko hayo, alisema kuwa atalifanyia kazi kwa kushirikiana na
mamlaka husika ili Wauguzi hao waweze kulipwa madai yao.
Hata hivyo Mapunda aliwashauri watumishi hao wa idara ya afya
waweke utaratibu wa kuanzisha chama chao cha akiba na mikopo, ili waweze kuondokana
na usumbufu kama huo wanaoupata sasa.
No comments:
Post a Comment