Na Steven Augustino,
Tunduru.
MFUKO wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) wilayani Tunduru
mkoa wa Ruvuma, unaendelea na zoezi lake la uhakiki wa kupitia taarifa za
wanufaika wake ikiwa ni jitihada ya kuweza kubaini kama kunawanufaika ambao
hawajakidhi vigezo husika na hatimaye waweze kuondolewa.
Juma Homera, Mkuu wa wilaya Tunduru. |
Hali hiyo imetokana na uwepo wa taarifa kwamba kuna baadhi ya
watoto ambao wamekwisha maliza shule, lakini bado wanaendelea kupokea fedha za
ruzuku kutoka katika mfuko huo.
Mshauri wa TASAF wilaya ya Tunduru, Christian Amani alisema
hayo wakati alipokuwa akizungumza na wanufaika wa vijiji vya Mkasale na Liwanga
vilivyopo tarafa ya Namasakata wilayani hapa.
Amani alisema kuwa tayari mfuko huo, umekwisha sambaza fomu maalum
za kufanya uhakiki huo kwa walimu wa shule zote za msingi na sekondari zenye
wanafunzi wanaonufaika na mpango huo ili kuweza kubaini, tatizo hilo lipo wapi
na hatimaye kulitafutia upembuzi yakinifu.
“Walimu wanaoshirikiana na wazazi kuficha taarifa za kumaliza
shule watoto wao hawana tofauti na wafanyakazi hewa, hivyo ni lazima hatua
zichukuliwe haraka ili kuweza kuwaondoa katika mfumo wetu wa utoaji ruzuku kwa
kaya maskini”, alisema.
Alisema katika zoezi hilo, TASAF haitamuonea mtu bali
itatekeleza majukumu yake kwa kuwapunguzia pato lao kulingana na idadi ya watoto
waliokuwa wakinufaika na mpango huo.
Naye Mratibu wa Mfuko huo wa maendeleo ya jamii wilaya ya
Tunduru, Stanley Haulle alisema kuwa katika utekelezaji wa zoezi hilo mkuu wa
kaya ambaye atabainika kuwa na watoto hewa wanaopokea ruzuku, atapunguziwa pato
lake kwa wastani wa shilingi 2,000 kwa kila mwezi hivyo kwa kaya iliyokuwa na watoto
wanne nayo itapunguziwa shilingi 16,000.
Aliongeza kuwa katika utekelezaji wa zoezi hilo, awali waliweza
kuondoa kaya maskini 484 zisizokuwa na sifa baada ya kujiridhisha hawakukidhi
vigezo husika.
No comments:
Post a Comment