Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
HALMASHAURI ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, imetoa
shukrani kwa Wadau wa maendeleo wilayani humo, kwa kutoa msaada wa magari ambayo
yametumika kubebea madawati kutoka mjini Songea mkoani humo kwenda wilayani hapa,
kwa ajili ya kukalia wanafunzi darasani.
Wilaya hiyo imepata mgawo wa madawati 537 ambayo
yametengenezwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Mlale mkoani hapa, kupitia fedha
za mfuko wa jimbo ambazo hutolewa na serikali kwa ajili ya shughuli mbalimbali
za maendeleo ya wananchi.
Emmanuel Kapinga ambaye ni Ofisa utumishi wa wilaya ya
Mbinga, alitoa shukrani hizo kwa niaba ya Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya
wilaya hiyo Gumbo Samanditu, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa
habari ofisini kwake juu ya mkakati wa kumaliza tatizo la madawati kama
ilivyoagizwa na Rais Dkt. John Magufuli.
“Upatikanaji wa madawati haya tumeweza kumaliza kabisa tatizo
la upungufu lililopo hapa wilayani kwetu, tunawashukuru wadau hawa wa maendeleo
hapa Mbinga kwa kutoa magari yao kwenda Songea kuchukua madawati haya ambayo
yametengenezwa na JKT kwa ajili ya kusaidia watoto wetu waweze kuandika
mwandiko mzuri wanapokuwa darasani”, alisema.
Kapinga alifafanua kuwa katika mkoa wa Ruvuma, halmashauri
yake imekuwa ya kwanza kuitika wito huo wa kwenda kuchukua madawati hayo licha
ya halmashauri zote mkoani humo, kupewa taarifa husika ya kwenda kuyachukua.
Hata hivyo aliongeza kuwa ufanisi huo umetokana na
ushirikiano mzuri uliopo kati ya uongozi wa halmashauri hiyo na wadau hao, hivyo
amewapongeza na kuwaomba waendeleze mahusiano hayo mazuri waliyonayo sasa ili
kuweza kuendelea kusukuma mbele gurudumu la maendeleo la wilaya hiyo kwa
manufaa ya wanambinga na taifa kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment