Na Steven Augustino,
Tunduru.
MADIWANI wa Chama Cha Wananchi (CUF) wilayani Tunduru mkoa wa
Ruvuma, wameahidi kuunga mkono kwa vitendo juhudi zinazofanywa na serikali ya
awamu ya tano, katika kuondoa kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wa wilaya
hiyo ili waweze kusonga mbele kimaendeleo.
Ahadi hiyo ilitolewa na Madiwani wa kata ya Nanjoka,
inayoongozwa na Rajab Mtimbalugono, kata ya Majengo, Abdallah Rajabu na diwani
wa kata ya Mlingoti Mashariki, Mohamed Aloyce.
Madiwani hao walisema hayo walipokuwa wakizungumza na Mkuu wa
wilaya ya Tunduru, Juma Homera alipowatembelea katika eneo la kufyatulia
matofari kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya shule ya msingi Umoja iliyopo mjini
hapa.
Diwani wa kata ya Nanjoka, Rajab Mkwawa alisema kuwa maamuzi
hayo wamefikia baada ya kubaini uwepo wa pungufu mkubwa wa miundombinu ya
kufundishia katika shule zilizopo katika maeneo yao na kwamba wamepanga
kufyatua tofari 60,000 ili kukidhi mahitaji ya ujenzi wa madarasa hayo.
Alisema kuwa baada ya kutambua tatizo hilo la upungufu
wa madarasa, wamefanya uhamasishaji kwa wananchi kuchangia nguvu zao, katika shule
zilizopo katika maeneo yao.
Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Umoja wilayani humo, Amina
Kachepa alifafanua kuwa shule hiyo ina wanafunzi 557 ambapo ina upungufu wa
vyumba vya madarasa sita, ofisi mbili, nyumba saba za kuishi walimu, vyoo
matundu 12 na madawati 162.
Akitolea ufafanuzi wa taarifa hiyo, Kachepa alimweleza Mkuu
wa wilaya ya Tunduru, Homera kuwa wanafunzi hao wamekuwa wakisoma chini ya miti
nyakati za kiangazi kutokana na upungufu wa madarasa na kwamba nyakati za
masika wamekuwa wakisoma kwa mtindo wa kupokezana katika vyumba hivyo vya
madarasa vilivyopo sasa.
Akijibu kero hizo Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Homera pamoja na
kupongeza jitihada hizo zinazofanywa juu ya ujenzi wa madarasa hayo alisema serikali
nayo itaendelea kuunga mkono jitihada hizo, kwa kununua vifaa vya kiwandani ili
ujenzi uweze kukamilika kwa wakati pale utakapoanza kufanyika.
Homera alisema kuwa kitendo cha viongozi na wananchi hao kuonesha
moyo wa kujitoa na kujitolea katika kazi hiyo, wanatakiwa kuhakikishiwa usalama
wa maisha na mazingira bora ya kufundishia.
No comments:
Post a Comment