Wakurugenzi Watendaji
wa Halmashauri, Miji, Manispaa na Majiji 185 hapa nchini wakila kiapo cha
maadili ya viongozi leo Ikulu Jijini Dar es salaam.
|
IKULU JIJINI DAR ES SALAAM,
WAZIRI Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim
Majaliwa amewataka Wakurugenzi watendaji wateule kuwa makini katika utekelezaji
wa majukumu yao ya kazi za kila siku, huku akiwatahadharisha kwamba wasije
wakajikuta wanaingia kwenye migogoro ya kifedha na kikazi dhidi ya watendaji
wengine pamoja na wananchi wanaoenda kuwaongoza.
Hayo yalisemwa na Waziri Mkuu Majaliwa alipokuwa akizungumza
na leo na Wakurugenzi watendaji wateule 185 wa majiji, manispaa, miji na
halmashauri za wilaya na kuwataka pia huko waendako waende wakafanye kazi
kwenye maeneo yao mapya waliyopangiwa kwa kuzingatia uadilifu, uwajibikaji na
uaminifu.
Waziri Mkuu ametoa wito huo leo, kabla hawajatoa viapo vya
maadili katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.
“Jukumu mlilopewa na Mheshimiwa Rais ni nyeti na linahitaji
utulivu wa kujituma kwa kila mmoja wenu, mnatakiwa mkafanye kazi kwa uadilifu
mkubwa kwa kila mmoja wenu kuwajibika ipasavyo”, alisema Majaliwa.
Majaliwa aliongeza kuwa wao ndiyo injini ya maendeleo katika
halmashauri zote hapa nchini katika kusimamia fedha za miradi ya maendeleo ya
wananchi, hivyo wanapaswa kuhakikisha wanasimamia fedha za ndani na fedha
zinazotoka serikali kuu, juu ya matumizi yake kwa lengo la kupata value for
money.
“Mkifika huko ninawasihi mshirikiane na wadau wengine ambao
ni wakuu wa mikoa, wilaya, kamati za ulinzi na usalama, wakuu wa idara,
watumishi wa idara mbalimbali zilizopo chini yenu na watendaji wa kata na
vijiji ili tuweze kufikia malengo yetu tuliyojiwekea ya kuwaletea maendeleo
wananchi”, alisisitiza.
Pia aliwaagiza kwa kuwataka wasome taarifa mbalimbali ili
waelewe majukumu na mipaka yao ya kazi, maeneo ya utawala na wajipange kikamilifu katika kusimamia na
kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwani imebeba ahadi zilizotolewa
na Rais aliyekuwa madarakani sasa, pamoja na Makamu wake wa Rais wakati wa
kampeni za uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan aliwataka
wateule hao watambue pia dhamana waliyopewa kuwa viongozi wa halmashauri na
kwamba wanakwenda huko kuwa watumishi wa umma na siyo watawala.
“Wewe ni kiongozi hivyo unapaswa kutengeneza watu wako ili
wakusaidie kutekeleza kile ulichotumwa kufanya, fanyeni kazi kwa bidii hivi
sasa Tanzania yetu inaenda kwa spidi kali lakini pia mjihadhari na kashfa za
matumizi mabaya ya fedha. Msisahau kuwa fedha ni fedheha, ukiitumia vibaya
utapata fedheha”, alisema.
Vilevile akiwahutubia wateule hao, Rais Dkt. John Magufuli
aliwataka huko waendako wakawe watatuzi wa kero za wananchi badala ya kuwatengenezea
migogoro isiyokuwa ya lazima na kuleta kero na matatizo yatakayoweza
kufarakanisha jamii, na kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi.
“Kaondoeni kero kwa wananchi wa hali ya chini, wako huko
wanatozwa kodi ndogo ndogo hata za kuuza mchicha, mtu akivuna mpunga wa kula
nyumbani kwake pia anatozwa kodi ni lazima kodi hizi mkazuie kwa sababu
tuliahidi kupunguza kero kwa wananchi na siyo kuongeza kero kwao,” alisisitiza.
Alisema ana imani nao kwamba wataenda kutekeleza ilani ya CCM
na akawataka waandae mipango yao ya maendeleo kila mmoja kulingana na eneo analolitawala
kwa kuitekeleza na sio vinginevyo.
Alisema katika mpango wa maendeleo wa miaka mitano, Serikali
imedhamiria kujenga Tanzania yenye uchumi wa viwanda na kuwataka wasimamie
kilimo ili mazao yatakayozalishwa yaweze kusindikwa hapa nchini.
No comments:
Post a Comment