Na Kassian Nyandindi,
Songea.
MIILI ya watu wawili wanaohofiwa kufa maji katika mto Ruvuma,
baada ya boti walilokuwa wakisafiria, imekutwa ikielea kando kando ya mto huo katika
kijiji cha Mitomoni wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma.
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Zubery Mwombeji ameitaja
miili ya watu hao kuwa ni Fadhil Hamis (9) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la
pili, shule ya msingi Mitomoni na Omary Jela (11) ambaye naye ni wa darasa la
tatu katika shule hiyo.
Alifafanua kuwa miili hiyo imepatikana juzi kwa nyakati tofauti
ambapo mwili wa kwanza wa Fadhil Hamis ulipatikana majira ya saa 12 asubuhi,
ukiwa unaelea juu ya maji jirani na kingo hizo za mto Ruvuma ambapo mwili wa
pili wa Omary Jela ulikutwa ukiwa juu ya maji kwenye eneo la kijiji cha Mitomoni,
majira ya saa 2 asubuhi.
Alisema kuwa miili hiyo imepatikana kufuatia juhudi za kuitafuta
zilizofanywa na wananchi wa vijiji vya Nakawale wilayani Songea na Mitomoni
wilayani Nyasa ambapo tangu Julai 2 mwaka huu, ilipotokea ajali hiyo ya boti
kuzama na kusababisha watu tisa kufa maji.
Kamanda Mwombeji alisema kuwa mto Ruvuma ambao una mamba
wengi pia unakina kirefu na kwamba, juhudi zinaendelea za kuitafuta miili
mingine ambayo mpaka sasa haijapatikana.
Vilevile amewaomba wananchi wa vijiji ambavyo vipo kando
kando ya mto huo waone umuhimu wa kuendelea kujenga ushirikiano na wenzao wa
vijiji vya Nakawale Songea, pamoja na Mitomoni wilayani Nyasa kuitafuta miili
ya watu saba ambayo bado haijapatikana.
No comments:
Post a Comment