Na Yeremias Ngerangera,
Namtumbo.
MKUU wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Luckness Amlima
ameshitushwa na taarifa ya uraia wa nchi mbili Msumbiji na
Tanzania ambao unafanywa na wananchi wa kijiji cha Likuyumandela, kata ya
Likuyu wilayani humo bila kufuata taratibu husika.
Amlima alishitushwa na taarifa hiyo wakati wa ziara yake ya
kikazi wilayani humo, ambayo ilienda sambamba na kuzungumza na wajumbe
wa baraza la maendeleo la kata katika kata zote za wilaya ya Namtumbo.
Luckness Amlima katikati, akiwa na kamati yake ya maendeleo. |
Akisoma taarifa ya maendeleo kata ya Likuyu kwa Mkuu wa
wilaya huyo, Mratibu elimu kata, Ireneus Fusi alisema kuwa pamoja na
changamoto zingine kuwepo lakini kata hiyo inachangamoto kubwa kwa
wananchi wake, kuwa na makazi ya kuhamahama ambapo wakati mwingine wanaishi
Tanzania au Msumbiji.
Fusi alifafanua kuwa hali hiyo ya kuhamahama imekuwa
ikiwayumbisha watoto wao hasa kwa wale ambao ni wanafunzi, wanaosoma shule za
msingi na sekondari.
Alisema kuwa katika kipindi cha mwaka huu, tayari wanafunzi
tisa wa darasa la saba shule ya msingi Mandela kata ya Likuyu ambao
wanatarajia kufanya mtihani wa taifa darasa la saba,
wametorokea nchi ya Msumbiji.
Kufuatia hali hiyo, Ofisa uhamiaji wa wilaya ya Namtumbo
Ditrick Kamuhabura alimweleza Mkuu wa wilaya ya Namtumbo, Amlima kuwa ofisi
yake ya uhamiaji itapiga kambi katika kata hiyo ili kuweza kujiridhisha kama
kweli kuna wananchi wanaishi nchi jirani ya Msumbiji na wakati mwingine
Tanzania bila kufuata taratibu husika.
Kamuhabura aliongeza kuwa kijiji cha Likuyumandela,
kimetokana na wakimbizi wa Msumbiji hivyo ofisi yake itafanya
mawasiliano na serikali ya nchi hiyo ili kujiridhisha juu ya jambo hilo, kama
wananchi hao wanauraia wa nchi mbili au la.
Hata hivyo kwa upande wake Mkuu wa wilaya hiyo, Amlima
alisema kuwa endapo kutakuwa na ukweli juu ya tatizo hilo ofisi yake
itawataka wananchi hao kuukana uraia wa nchi moja na sio vinginevyo.
No comments:
Post a Comment