Na Steven Augustino,
Tunduru.
SERIKALI wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, imewataka viongozi
wanaounda vikundi ambavyo vimekuwa vikitishia amani katika wilaya hiyo na
kuvuruga dini ya kiislam kuacha mara moja tabia hiyo, vinginevyo watachukuliwa
hatua za kisheria dhidi yao.
Aidha imewakumbusha kutekeleza majukumu yao kwa kufuata
maelekezo yaliyopo katika katiba inayosimamia utekelezaji wa majukumu ya dini yao,
chini ya mwamvuli wa baraza linalosimamia maudhui ya dini hiyo (BAKWATA).
Mkuu wa wilaya ya Tunduru Juma Homera alisema hayo juzi,
wakati alipokuwa akimwakilisha Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith
Mahenge kwenye sherehe za baraza la Idi
Elfitry zilizofanyika kimkoa wilayani hapa.
Homera alisema kuwa serikali inazo taarifa juu ya uwepo wa
vikundi hivyo, pamoja na kazi wanazozifanya na kwamba ili kufikia ufumbuzi
imepanga kufanya mazungumzo na viongozi wake, ili kuwaonya wasiendelee na tabia
hiyo.
Awali akisoma risala katika maadhimisho hayo, Sheikh Omary
Machundo alimweleza Mkuu wa wilaya Homera kuwa, miongoni mwa changamoto
zinazotishia kuvuruga amani na dini ya uislamu wilayani humo ni uwepo wa vikundi
hivyo visivyojulikana.
Alisema kuwa viongozi wa vikundi hivyo wamekuwa na tabia ya
kuandika nyaraka mbalimbali, zenye kuyaruhusu baadhi ya makundi kutoka mataifa ya
nje nchi kuingia katika wilaya za mkoa wa Ruvuma, wakisingizia kueneza dini jambo
ambalo ni hatari kwa usalama wa nchi.
No comments:
Post a Comment