Na Kassian Nyandindi,
Songea.
WATU tisa wanahofiwa kufa maji katika mto Ruvuma mkoa wa
Ruvuma, kati ya 45 waliokuwa kwenye boti walilokuwa wakisafiria wakivuka mto
huo kutoka kijiji cha Nakawale kata ya Muhukuru wilaya ya Songea, wakielekea
kijiji cha Mitomoni wilayani Nyasa mkoani humo.
Zubery Mwombeji. |
Aidha katika boti hilo wanaohofiwa kupoteza maisha ni kwamba,
watano ni wanafunzi wa shule ya msingi Mitomoni na wa nne ni wakazi wa kijiji
hicho wilayani humo, ambapo wakati wanavuka mto huo imeelezwa kuwa boti
lilizima injini yake ghafla na kusababisha maafa hayo.
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji alimweleza
mwandishi wetu kuwa tukio hilo lilitokea majira ya usiku wa kuamkia Julai 3
mwaka huu na sehemu waliyokuwa wakivuka kwenye mto huo ina urefu wa mita 50.
Mwombeji aliwataja wanaohofiwa kufa maji na miili yao bado
haijapatikana kuwa ni wanafunzi wa shule ya msingi Mitomoni ambao ni Awetu
Shaibu (14) wa darasa la sita, Omary Waziri (13) darasa la nne na Fadhil Hamis
(9) wa darasa la pili.
Wanafunzi wengine ni Omary Jella (11) wa darasa la pili,
Zulpha Ally (14) anayesoma darasa la nne na kwamba wengine ambao ni wakazi wa
kijiji cha Mitomoni kuwa ni Fatuma Said (41), Rajabu Machupa (17), Tupishane Mustapha
(5) na Stumai Abdallah ambaye ni mtoto mchanga mwenye umri wa miezi mitano.
Pia Kamanda huyo wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Mwombeji
alifafanua kuwa Kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa huo ilikwenda katika eneo
la tukio na kuunda kikosi ambacho kinashirikiana na wananchi wanaoishi vijiji
vya jirani na tukio lilipotokea kufanya kazi, ya kuendelea kutafuta miili ya
watu hao wanaohofiwa kufa maji.
No comments:
Post a Comment