JAJI Mkuu, Mohammed Chande Othman, amesema Mahakama Maalumu
ya Uhujumu Uchumi na Ufisadi itaamua kesi kwa muda usiozidi miezi tisa na
kwamba itaanza na majaji 14.
Aidha, wameandaa kozi maalumu kwa majaji 14 watakaofanya kazi
katika mahakama hiyo itakayoanza Julai 11 hadi 15, mwaka huu, kwenye Chuo cha
Mahakama Lushoto mkoani Tanga, ili kupeana mwongozo juu ya uendeshaji wa
mahakama hiyo.
Jaji Mkuu alisema, kesi zitakazoendeshwa katika mahakama hiyo
ni zile ambazo upelelezi wake umekamilika ili uamuzi utolewe mapema. Kwa mujibu
wa Jaji Mkuu, dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kupambana na uhalifu huo.
Aliyasema hayo jana wakati alipotembelea Maonesho ya 40 ya
Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam yanayoendelea kwenye Viwanja vya Mwalimu
Nyerere vilivyopo katika Barabara ya Kilwa, ambayo alisema yamezidi kuwa bora
kuliko miaka mingine.
Alisema baada ya sheria hiyo ya uhujumu uchumi kupitishwa na
Bunge, imekuwa na marekebisho mengi na kuboreshwa kwa kiasi kikubwa.
Jaji Mkuu alisema pia, hatua inayofuata ni Rais kutoa idhini
ya sheria hiyo na baadaye kupitishwa kwa kutangazwa katika Gazeti la Serikali
ili ianze kutumika.
Alieleza kuwa baada ya kutangazwa katika Gazeti hilo la
Serikali, Jaji anatakiwa kutunga kanuni mbalimbali, mojawapo ikiwa ya kulinda
mashahidi kutokana na kuwa sheria hiyo inahusu makosa makubwa na hatari ya
ugaidi, rushwa na uhujumu uchumi.
“Tuko mbioni kutunga kanuni hizo na kuhakikisha mashahidi
wanalindwa. Jengo la mahakama hii litakuwa katika Chuo cha Sheria karibu na
Mlimani City na tayari tumepeleka wasajili watendaji,” alisema.
Mwishoni mwa wiki, Jaji Mkuu huyo alisema kuwa majengo ya
mahakama hiyo yatakabidhiwa leo. Kutokana na maelezo yake, Mahakama iko tayari
kuendesha divisheni hiyo, baada ya kukabidhiwa majengo hayo.
Alisema wataanza kutoa semina kwa majaji na watumishi wengine
wa mahakama hiyo juu ya namna divisheni hiyo itakavyoendesha shughuli
zake.
Aidha, aliweka wazi kuwa hadi sasa hakuna kesi hata moja
iliyokwishatambuliwa kwamba itashughulikiwa na mahakama hiyo.
No comments:
Post a Comment