Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
JAMII imetakiwa kuwalea, kuwatunza na kuwajali watu wenye ulemavu
wa ngozi albino kwa kuhakikisha kwamba wanaishi katika mazingira mazuri, yenye
usalama na sio kuwanyanyapaa pale wanapohitaji mahitaji yao ya msingi.
Aidha Chama Cha Walemavu Tanzania (CHAWATA) tawi la Mbinga
mkoa wa Ruvuma kimeshauriwa kuendelea kushirikiana na serikali, ili walemavu
hao pia waweze kupata elimu juu ya afya ya usalama wa ngozi pamoja na kutatua
matatizo mbalimbali yanayowakabili katika maisha yao.
Hayo yalisemwa na Katibu tawala wa wilaya ya Mbinga, Mhandisi
Gilbert Simya wakati alipokuwa akipokea msaada wa mafuta maalum ya kupaka watu
wenye ulemavu wa ngozi albino katika hafla fupi iliyohudhuriwa na walemavu hao
ambayo ilifanyika kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo uliopo mjini hapa.
Mafuta hayo yalitolewa na Chama hicho cha walemavu kwa watu
87 wenye ulemavu wa ngozi Halmashauri ya mji wa Mbinga, baada ya kuyapokea
kutoka kitengo cha magonjwa ya ngozi Hospitali ya KCMC Moshi mkoani Kilimanjaro ambayo
yanathamani ya shilingi 870,000.
“Nampongeza Mwenyekiti wa CHAWATA ndugu Martin Mbawala kwa
jitihada zake alizozifanya juu ya namna ya kupata mafuta haya, kama chama
endeleeni kuwa wabunifu namna ya kulisaidia kundi hili tete la walemavu kwa
kuwalea na kuwatunza katika mazingira mazuri”, alisisitiza Mhandisi Simya.
Vilevile Simya aliongeza kwa kuwataka viongozi wa chama hicho
kutumia fursa waliyopewa na wanachama wao, kuhakikisha kwamba wana ainisha
matatizo waliyonayo walemavu wa Mbinga na kuyafikisha katika ofisi za serikali
ili yaweze kufanyiwa kazi.
Awali akitoa maelezo mafupi juu ya changamoto zinazowakabili albino
katika Halmashauri ya mji huo, Mwenyekiti wao Gelioni Nchimbi ambaye ni wa
Chama cha maalbino alisema kuwa wanashindwa kuwafikia wanachama wake kwa
urahisi kutokana na kukosa usafiri na rasilimali fedha, kwa ajili ya
kuwatimizia mahitaji yao ya msingi.
Nchimbi alifafanua kuwa kukosekana kwa fedha kunakwamisha
utendaji kazi na uendeshaji wa shughuli husika, hivyo wanaiomba serikali kuwaangalia
kwa jicho la huruma kwa kutatua kero zinazowakabili ili kundi hilo tete liweze
kusonga mbele kimaendeleo.
No comments:
Post a Comment