Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.
BAADHI ya wananchi wa wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, wamesema
kwamba wanapata adha kubwa na hufikia hatua ya kushindwa kufanya shughuli zao mbalimbali
za kimaendeleo, kutokana na ukosefu wa huduma ya vituo vya kuuza mafuta katika wilaya
hiyo.
Aidha wameomba watu wenye uwezo mkubwa wa kifedha, kujitokeza
kwenda wilayani humo kuwekeza katika sekta hiyo muhimu hatua ambayo itarahisisha
upatikanaji wa huduma hiyo na kuharakisha kukua kwa shughuli zao za
kiuchumi.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wenzake, mkazi mmoja wa mji
wa Mbamba bay wilayani Nyasa Petro Ndembele alisema kuwa wilaya hiyo tangu
ianzishwe mwaka 2013 hakuna huduma ya vituo vya kuuza mafuta, jambo ambalo linachangia
kwa kiasi kikubwa maisha ya wakazi wengi wilayani hapa kuwa magumu sambamba na
kuongezeka kwa nauli kutoka sehemu moja kwenda nyingine katika magari ya
kusafiria abiria na kuwafanya waendelee kuwa maskini.
Ndembele alisema kuwa ukosefu huo wa mafuta husababisha
kushindwa kuwaokoa hata ndugu zao, pale yanapotokea maafa ndani ya Ziwa Nyasa
kwani hushindwa kuwafikia kwa haraka kwa kutumia boti, maeneo ya ajali
inapotokea na kulazimika kutumia muda mrefu kuwatafuta ndugu na jamaa zao ambao
hupoteza maisha katika ziwa hilo.
Kwa mujibu wa Ndembele alisema endapo kungekuwepo vituo
maalumu vya kuuzia mafuta badala ya utaratibu unaotumika sasa, ambapo wafanyabiashara
wachache kutoka wilaya jirani ya Mbinga wanakwenda kufanyabiashara hiyo kwa
kutumia maguduria na ndoo, ambavyo vinachangia kupunguza ubora wa mafuta hayo
kutokana na baadhi yao kuwa na tabia ya kuyachakachua.
Pia amepongeza juhudi kubwa za serikali ya awamu ya tano
inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli ya kupambana na vitendo vya wizi, ufisadi
na uzembe kwa watumishi wa umma hasa kwa wale waliozoea kufanya kazi kwa mazoe
huku wakijifanya wao ni miungu watu, kwani hatua hiyo itasaidia kuharakisha
upatikanaji wa huduma za kijamii na suala zima la kukuza maendeleo katika
maeneo mbalimbali hapa nchini.
Alisema kuwa hata kukosekana kwa huduma za kijamii kwa
baadhi ya maeneo hapa nchini, kumechangiwa na watumishi ambao walifanya kazi
kwa ajili ya kujinufaisha matumbo yao, kwani fedha ambazo walizitumia kwa ajili
ya maslahi yao binafsi zingewezesha kupeleka huduma husika kwa wananchi
hasa wa maeneo ya vijijini.
Kwa upande wa suala la uhaba wa madawati kwa shule za msingi
na sekondari hapa nchini, Ndembele alisema tatizo hilo limesababishwa na uzembe
uliofanywa na baadhi ya watumishi waliopewa
dhamana ya kusimamia rasilimali za nchi na kuzitumia vibaya, huku wakiacha kwa
makusudi kutatua shida na kero za Watanzania wengine ambapo amemuomba
Rais Magufuli kuendelea kuwatumbua watumishi hao ambao wanaifilisi nchi
yetu.
Hata hivyo amewataka wananchi kutumia muda wao kufanya kazi
za kujiletea maendeleo, badala ya kutumia muda mwingi kufanya anasa kwa sababu
jambo hilo limekuwa likichangia umaskini licha ya Tanzania kubahatika kuwa
na rasilimali nyingi ambazo hadi sasa bado hazijatumika kikamilifu kwa ajili ya
kujipatia maendeleo.
No comments:
Post a Comment