Na Kassian Nyandindi,
Songea.
KAMPUNI ya Mantra Tanzania, imekabidhi madawati 500
yenye thamani ya shilingi milioni 40 kwa Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith
Mahenge ikiwa ni mwitikio wa agizo la Rais Dkt. John Magufuli kwa wadau
mbalimbali wa ndani na nje ya nchi, kuchangia utengenezaji wa madawati hayo ili
kuweza kukabiliana na upungufu uliopo katika shule za msingi na sekondari hapa
nchini.
Msaada huo unafuatia uamuzi wa serikali ya awamu
ya tano wa kutoa elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne
kwa wanafunzi ambao hapo awali walikuwa wanakosa haki ya kupata elimu, hatua
ambayo imechangia ongezeko kubwa la wanafunzi darasani na kusababisha uhaba
mkubwa wa madawati.
Mbali na upungufu wa madawati pia imesababisha
kuwepo kwa uhaba wa vifaa vya muhimu mashuleni ikiwemo viti, meza, vitabu na
baadhi ya vifaa vingine kwa ajili ya matumizi ya wanafunzi hivyo serikali inaendelea
kuwaomba wadau hao kutoa michango yao ili kufikia malengo ya ufumbuzi wa
tatizo hili na kwamba serikali ya mkoa wa Ruvuma, iliiomba kampuni ya Mantra
Tanzania na wadau wengine wa mkoa huo kuchangia madawati hayo kwa lengo la
kuweza kukabiliana na tatizo hilo.
Mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo, Frederick
Kibodya alisema kuwa msaada huo wa madawati umetolewa kwa lengo la kuunga mkono
jitihada zinazofanywa na Rais John Magufuli kwa kutoa elimu bure ya msingi
na sekondari hapa nchini, kwa kuongeza pia ubora wa elimu na kuboresha
mazingira ya kusomea wanafunzi.
Alisema kampuni ya Mantra inaamini kwamba,
madawati hayo yatatoa mchango chanya katika kuleta ari ya kujifunza kwa watoto
1,500 na kuwahamasisha kwenda shule kila siku, kushiriki kikamilifu masomo yao na
kuandika mwandiko mzuri tofauti na kukaa chini sakafuni.
Kwa mujibu wa Kibodya ni kwamba, Mantra ina imani
kwamba mchango huo wa madawati 500 utachangia pia katika kuboresha kiwango cha
elimu mkoani Ruvuma, ambako inaendesha shughuli zake.
Kibodya alieleza kuwa tangu kampuni hiyo ianze utafiti wa madini
aina ya Urani katika mradi wake wa Mkuju, wilayani Namtumbo mkoani humo imekuwa
na jitihada ya kuendelea kuchangia na kuboresha mazingira ya upatikanaji wa elimu
bora kwa kuchangia madawati, vitabu kwa baadhi ya shule za sekondari.
Vilevile wameweza kujenga miundombinu ya umeme wa nishati ya
jua, ujenzi wa maabara ya sayansi katika shule hizo ambapo mbali na hayo,
Mantra pia imekuwa ikisaidia kuboresha mazingira na sekta ya afya wilayani Namtumbo
na Tanzania kwa ujumla.
Kampuni ya Mantra inatekeleza pia mpango wake wa kupambana na
ujangili kwa kutambua tembo wa Tanzania ndio miongoni mwa wanaouawa hivyo
katika kutekeleza jambo hilo, imechukua hatua kwa kuzindua operesheni kali na
ya teknolojia ya juu katika kupambana na ujangili huo kwa kushirikiana na idara
ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Aliongeza kuwa kampuni hiyo ambayo inamiliki mradi huo wa
Urani katika mto Mkuju wilayani Namtumbo ni kampuni tanzu ya Uranium One
na shirika lake kuu la ROSATOM, ambalo ni shirika la nishati ya Atomiki la
serikali ya Urusi na kampuni ya Uranium One ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa
wa urani duniani ikiwa na umiliki wa aina mbalimbali katika nchi za Kazakhstan,
Marekani, Australia na Tanzania.
No comments:
Post a Comment