Wananchi wa kata ya Mbalatse wilayani Makete mkoa wa Njombe, wakiwa wameandamana kutaka ardhi yao iliyochukuliwa na mwekezaji. (Picha kwa hisani ya ITV) |
Na Kassian Nyandindi,
Njombe.
MBUNGE wa Jimbo la Makete mkoa wa Njombe, Profesa Norman
Sigala amesema kwamba anasikitishwa na kitendo cha uongozi wa mkoa huo
kufumbia macho kwa muda mrefu malalamiko ya wananchi wake, juu ya kutwaliwa
ardhi yao na mwekezaji wa kampuni ya Silverlands Tanzania bila kufuata taratibu
husika, jambo ambalo linahatarisha kutokea kwa machafuko kati ya wananchi na
mwekezaji huyo.
Mbunge huyo ambaye ni wa kupitia tiketi ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) alisema kuwa licha ya kero hiyo kufikishwa mezani kwa viongozi
wa ngazi ya mkoa huo hakuna hatua zinazoonesha kuzaa matunda hivyo kuna kila
sababu kwa serikali, kuchukua hatua za haraka ili kuweza kunusuru hali hiyo
isiweze kuleta madhara hapo baadaye.
Hayo yalisemwa na Profesa Sigala alipohojiwa na waandishi wa
habari ambao walitembelea katika kata ya Mbalatse wilayani Makete, kwa lengo la
kutaka kujua juu ya hatma ya mgogoro wa ardhi ambao umedumu kwa muda mrefu sasa
kati ya wananchi na mwekezaji huyo.
Alisema kuwa tangu mwaka 1980 mwekezaji huyo aliingia katika
kata ya Mbalatse kwa ombi la kupewa ardhi ekari 70 ili aweze kufanya utafiti wa
kilimo cha zao la shairi, lakini anashangaa kuona kwamba amemilikishwa eneo la
hekta zaidi ya 3,000 bila kufuata taratibu za uchukuaji wa maeneo ya wananchi
wake kama sheria za nchi zinavyotaka.
“Nasikitishwa sana na kitendo kinachofanywa na uongozi huu wa
mkoa kutoshughulikia mgogoro huu wa ardhi ili uweze kwisha kwa wakati na
madhara yasiweze kutokea hapo baadaye, wananchi wa Mbalatse wanajua kwamba
ardhi yao inatumika kwa manufaa ya watu binafsi sio kwa manufaa ya taifa, hivyo
kupokwa kwa ardhi hii zimetumika njia za ujanja ujanja na udanganyifu mkubwa”,
alisema.
Naye Diwani wa Kata ya Mbalatse, Edson Msigwa alifafanua kuwa
hata uongozi wa kata hiyo haujui chochote kinachoendelea katika mashamba hayo
kufuatia ulinzi mkali ambao umewekwa na mwekezaji huyo, ambapo walinzi waliopo
muda wote usiku na mchana wamekuwa na silaha za moto ili kuzuia mtu yeyote
asiweze kuingia katika eneo hilo.
Kadhalika Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Makete
Egnatio Mtawa alipohojiwa, alikiri kuwepo kwa mgogoro huo na
kuongeza kuwa tayari hatua zimeanza kuchukuliwa tume imeundwa kuchunguza kwa
undani juu ya jambo hilo, ambapo baadaye itatoa taarifa baada ya kumaliza kazi
yake.
Naye Meneja wa shamba la Kampuni ya Silverlands Tanzania,
Steven Maina alipoulizwa juu ya jambo hilo alisema kuwa ndani ya eneo hilo wao
wana hati miliki na kwamba kuna kiwanja cha ndege ambacho kimekuwa kikitumika
ndege kutua kipindi cha kiangazi, wakati wa mavuno ya zao hilo na kwamba pia
kumejengwa majengo ya ofisi na nyumba za kuishi wafanyakazi wa shamba hilo.
Maina alifafanua kuwa sehemu ya shamba hilo kumezalishwa pia zao
la shairi alizeti, ngano na mboga mboga pamoja na miti ya asili na kwamba haoni
sababu ya mgogoro huo kuendelezwa huku akishauri kwamba kuna kila sababu ya
serikali kuchukua hatua ya kumaliza tofauti zilizopo.
Hata hivyo Mkuu wa mkoa wa Njombe, Dkt. Rehema Nchimbi
alipotakiwa kutolea ufafanuzi juu ya hali hiyo aliwataka waandishi wa habari
kwenda kumuona Afisa mipango miji wa mkoa huo Sarah Seme, ambapo baada ya
kuonana naye alikanusha uwepo wa mgogoro huo wa ardhi katika kata ya Mbalatse
na kuongeza kuwa wananchi wa kata hiyo wanataka shamba hilo linaloendeshwa na
mwekezaji huyo lirejeshwe mikononi mwao, ili waweze kuzalisha mazao yao ya aina
mbalimbali.
No comments:
Post a Comment