Wednesday, July 6, 2016

MSONGOZI ATOA MSAADA WA KADI ZA MATIBABU KWA WANAWAKE WA UWT RUVUMA



Na Julius Konala,
Songea.

MBUNGE wa viti maalumu wanawake kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Ruvuma, Jacqline Msongozi ametoa msaada wa kadi kwa ajili ya huduma za matibabu (CHF) kwa wajumbe 30 wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT) wa wilaya ya Songea mkoani humo.

Msaada huo ambao unathamani ya shilingi 300,000 umetolewa juzi na Mbunge huyo, wakati alipokuwa akizungumza katika kikao cha baraza la wanawake hao kwa lengo la kuwashukuru kwa kumchagua kuwa mwakilishi wao, kilichofanyika mjini hapa.

Jaqcline Msongozi.
Akizungumza katika kikao hicho, Jaqcline amewataka wanawake hao kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kwa kuhamasishana kujiunga na mfuko wa bima ya afya, ili waweze kuondokana na mzigo wa gharama kubwa za matibabu pale wanapougua.

“Taifa lenye wananchi wagonjwa haliwezi kupiga hatua mbele ya kimaendeleo nawataka hakikisheni mnajiunga na mfuko huu wa bima ya afya, pamoja na kujiunga kwenye vikundi vya ujasiriamali kwa lengo la kuinua uchumi wenu na Taifa letu kwa ujumla”, alisema.

Kikao hicho kilikwenda sambamba na mafunzo ya elimu ya ujasiriamali, yaliyokuwa yakiendeshwa na wataalamu wa kutoka Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) mjini Songea, pamoja na elimu ya kujiunga na mfuko wa bima ya afya ambayo yaliwezeshwa na Mbunge huyo.


Aidha alisisitiza kwa kuwataka wanawake hao, kutumia vyuo vya ufundi stadi kwa lengo la kujipatia ujuzi wa ushonaji wa nguo, upambaji, upishi pamoja na shughuli nyingine za ufugaji wa kuku wa mayai.

Naye Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Songea, Marry Duwe aliwataka wanawake hao pia kujikita katika shughuli mbalimbali za maendeleo, kuvunja makundi na badala yake watoe ushirikiano kwa viongozi wao ili kuweza kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Kwa upande wao baadhi ya wajumbe wa kikao hicho wamempongeza Mbunge huyo kwa moyo wake wa kukumbuka kupita kushukuru, kuwapa msaada wa kadi hizo za matibabu pamoja na kuwapatia mafunzo ya ujasiriamali na mfuko wa bima ya afya.

No comments: