Naibu
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Mhandisi Stella Manyanya
akiangalia ramani ya kiwanja cha ujenzi wa chuo cha VETA wilayani Namtumbo mkoa
wa Ruvuma. (Picha na Moses Konala)
|
Na Yeremias Ngerangera,
Namtumbo.
IMEELEZWA kuwa serikali hapa nchini, katika mwaka huu wa
fedha inatarajia kujenga vyuo vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi stadi (VETA)
katika wilaya ya Njombe, Ludewa, Geita na Namtumbo ikiwa ni
lengo la kuwasogezea wananchi huduma husika kwa manufaa ya kizazi cha sasa na
kijacho.
Aidha katika wilaya hizo ambako ujenzi huo utafanyika,
viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia suala hilo wametakiwa kujenga
ushirikiano na kuhakikisha kwamba, ujenzi huo unakamilika kwa wakati ili kuweza
kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Stella Manyanya
alisema hayo juzi alipokuwa kwenye ziara yake ya kikazi wilayani Namtumbo
mkoani Ruvuma, kukagua eneo ambalo linatarajiwa kujengwa chuo hicho wilayani
humo.
“Nimeridhishwa na ukubwa wa eneo hili
lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa chuo hiki cha VETA
hapa Namtumbo, natoa agizo kwa viongozi wote wa wilaya ambako ujenzi huu
utafanyika kusimamia kikamilifu zoezi hili ili serikali iweze kufikia malengo
yake ya maendeleo tuliyojiwekea kwa wananchi wetu”, alisisitiza Manyanya.
Manyanya alimtaka pia Mkuu wa wilaya hiyo, Luckness Amlima
kushirikiana na wataalamu watakaopewa dhamana ya ujenzi wa chuo hicho kwa kuwa
wabunifu na kuelimisha jamii juu ya elimu itakayotolewa chuoni hapo mara ujenzi
utakapokamilika, itaendana na nyakati za viwanda na sio vinginevyo.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Namtumbo, Amlima alimhakikishia
Naibu Waziri huyo kwamba mara ujenzi huo utakapoanza atausimamia kwa
umakini mkubwa, ili adhma hiyo ya serikali iweze kufikia malengo yake.
Pamoja na mambo mengine, akitoa taarifa ya maendeleo ya eneo
linapojengwa chuo hicho cha mafunzo ya ufundi stadi, Afisa ardhi na maliasili
Maurus Hyera alifafanua kuwa eneo lililotengwa lina ekari 30
ambalo tayari limepimwa kwa ajili ya kuanza ujenzi huo.
No comments:
Post a Comment