Na Kassian Nyandindi,
Songea.
JESHI la Polisi mkoani Ruvuma, linamshikilia Justine Ambrose
Nchimbi (30) ambaye ni mtoto wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani
humo kwa tuhuma ya kumbaka mwanafunzi wa shule ya wasichana ya sekondari
Mbinga, iliyopo katika kata ya Kigonsera wilayani humo.
Aidha kwa mujibu wa taarifa zilizomfikia mwandishi wetu na
kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji zinaeleza kuwa
tukio hilo lilitokea Julai 2 mwaka huu majira ya usiku katika kijiji cha Kitai
wilayani hapa.
Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Ernest Mangu. |
Mwombeji alisema kuwa mwanafunzi huyo ambaye ana umri wa
miaka 14 anasoma kidato cha kwanza katika shule hiyo na kwamba
alibakwa na kijana huyo, ambaye ni mfanyakazi wa kukusanya mapato ya
halmashauri ya wilaya hiyo katika geti la Kitai ambapo alitumia nguvu kwa
kumvuta mtoto huyo na kumuingiza kwenye kibanda cha walinzi kilichopo katika
eneo hilo na kumfanyia unyama huo.
Alisema kuwa mtoto huyo wakati anafanyiwa kitendo hicho
alikuwa akitokea nyumbani kwake kijiji cha Ngingama kata ya Lituhi wilaya ya
Nyasa, ambapo alipanda basi na kushuka Kitai majira ya saa mbili usiku ili
aweze kusubiri magari yanayotokea Songea kwenda Mbinga na hatimaye aripoti
katika shule hiyo anayosoma ili aendelee na masomo yake.
Pamoja na mambo mengine, timu ya waandishi wa habari ambayo
iliwasili katika hospitali ya wilaya ya Mbinga ambako mtoto huyo amelazwa
kwenye wodi maalumu ya wagonjwa wa bima, imeshuhudia hali yake ikiwa mbaya huku
akizungumza kwa shida.
Mwanafunzi huyo aliwaeleza waandishi wa habari kuwa baada ya
kushuka basi nyakati hizo za usiku, wakati anasubiri basi lingine ili aweze
kuelekea katika shule hiyo anayosoma ndipo ghafla alitokea kijana aliyemtaja
kwa jina la Justine Ambrose Nchimbi na kumvuta kwa nguvu kwenye kibanda hicho cha
walinzi na kumbaka.
“Wakati anatumia nguvu ya kunivuta kuelekea kwenye kile
kibanda nilikuwa nikipiga kelele, yeye alikuwa akikazana kuniziba mdomo lakini
sikupata msaada wowote mpaka alipofanikisha kitendo chake cha kunifanyia unyama
huu”, alisema mtoto huyo.
Alifafanua kuwa baada ya kufanyiwa kitendo hicho alikuwa
akivuja damu nyingi jambo ambalo lilimfanya ashindwe kutembea kutokana na
maumivu makali aliyokuwa akiyapata na kulazimika kulala kwenye kibanda hicho
mpaka ilipofika majira ya asubuhi Julai 3 mwaka huu, ndipo aliomba msaada kwa
wasamaria wema ambao walimsafirisha kwa gari mpaka kituo kikuu cha Polisi
wilaya ya Mbinga na kwenda kupatiwa matibabu hospitalini hapo.
“Damu ziliendelea kunitoka kwa muda mrefu huku tumbo langu
likiwa linauma sana na sasa sehemu zangu za siri zimevimba bado najisikia
maumivu makali mama yangu mzazi alipowasili hapa, amenitolea damu chupa mbili
ambazo madaktari wameweza kunifanyia matibabu na kunusuru uhai wangu”, alisema
mtoto huyo huku akidondosha machozi.
Hata hivyo mganga mkuu wa hospitali ya wilaya ya Mbinga,
Elisha Robert alithibitisha juu ya mwanafunzi huyo kubakwa na kwamba
alipotakiwa kutolea maelezo ya kina juu ya hali ya mgonjwa huyo, alikataa na
kusema kuwa zitatolewa baadaye mara baada ya afya yake kurejea katika hali ya
kawaida.
No comments:
Post a Comment