Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
HALMASHAURI ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, imejiwekea
mikakati ya kuhakikisha kwamba miji midogo iliyopo katika halmashauri hiyo ardhi
yake inapimwa kisheria na kuwafanya wakazi waliopo katika maeneo husika,
wasiweze kujenga kiholela.
Aidha katika vijiji kupitia kamati zake, watashirikishwa juu
ya mamlaka ya taratibu husika za upangaji wa matumizi ya ardhi na kwamba
upimaji huo utashirikisha pia wananchi kwa kuchangia gharama ndogo.
Hayo yalisemwa juzi na Mthamini wa ardhi wilaya ya Mbinga,
Gabriel Kameka alipokuwa akitoa mafunzo elekezi ya siku moja kwa Madiwani wa halmashauri ya
wilaya hiyo, yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Umati uliopo mjini hapa.
Kameka alifafanua kuwa kwa kutambua hilo serikali iliandaa
sera ya ardhi mwaka 1995 pamoja na sheria zake, kwa madhumuni ya kuongoza
ugawaji juu ya matumizi bora ya ardhi na kulinda haki zote zilizopo ndani yake.
Alisema kuwa malengo ya semina hiyo ni kuwawezesha madiwani
huko waendako katika kata zao, wakaelimisha jamii na kuwezesha viongozi wengine
wa umma waweze kutambua juu ya faida za upangaji, upimaji na umilikishwaji wa
ardhi ndani ya miji midogo na vijiji.
“Viongozi wa umma mnapaswa katika hili kwenda kuhamasisha
wananchi na kuwezesha utafutaji, upatikanaji na utekelezaji wa sheria ya ardhi
ili jamii iweze kunufaika kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye”, alisema
Kameka.
Alifafanua kuwa lengo kuu la Wizara ya ardhi nyumba na
maendeleo ya makazi, ipo kwenye mpango wa kupima kila kipande cha ardhi na
kukimilikisha mpaka hapo ifikapo mwaka 2025.
Mthamini huyo wa ardhi wilaya ya Mbinga, Kameka alieleza kuwa
kwa kuzingatia hilo halmashauri hiyo inataka iwe ya kwanza kutekeleza agizo
hilo kwa kupima kila kipande cha ardhi, kilichopo katika miji midogo na vijiji
vyote ndani ya wilaya hiyo.
Pamoja na mambo mengine aliongeza kuwa katika kutekeleza
zoezi hilo, itamlazimu kila mmiliki wa ardhi kijijini kulipia gharama za
upimaji wa kipande chake cha ardhi ambapo
timu ya wataalamu wa halmashauri hiyo imependekeza kupunguza gharama hizo, ambazo
hapo awali ilikuwa ni shilingi 300,000 za upimaji ardhi kwa ekari moja na
kufikia shilingi 120,000 kutokana na kipato cha wananchi wake.
Kwa upande wao Madiwani wa halmashauri hiyo, walipongeza
juhudi hizo zinazofanywa na wataalamu wake huku wakiunga mkono na kueleza
kwamba watakwenda kuelimisha wananchi katika maeneo yao, ili zoezi hilo
litakapoanza kutekelezwa liweze kuwa na ufanisi mkubwa.
No comments:
Post a Comment