Na Julius Konala,
Songea.
MBUNGE wa jimbo la Songea mjini kupitia tiketi ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) mkoani Ruvuma, Leonidas Gama amesema kuwa mikopo inayotolewa na
taasisi za kifedha kwa riba kubwa, imekuwa ni kikwazo cha maendeleo ya wananchi katika kupambana na umaskini.
Leonidas Gama. |
Gama alisema hayo juzi wakati alipokuwa akizungumza na
vikundi mbalimbali vya wajasiriamali mjini hapa, ambavyo vinaratibiwa na Jumuiya
ya Mabinti wa Maria Immaculata (DMI) mjini Songea.
Alisema kuwa mikopo hiyo imekuwa sio msaada kwa wananchi,
badala yake imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa kuwaingiza katika dimbwi la
umaskini kutokana na baadhi yao wanaposhindwa kuirejesha, mali zao hunyang’anywa
na kuuzwa.
Kufuatia hali hiyo mbunge huyo, amewataka wananchi kujiunga
kwenye vikundi mbalimbali vya ujasiriamali ili waweze kupata mikopo inayotolewa
na serikali kwa riba nafuu.
Aidha amevipongeza vikundi vya ujasiriamali vinavyoratibiwa
na Jumuiya hiyo ya DMI, kwa kukidhi vigezo vya kukopesheka huku akiwataka pia
kutumia mikopo wanayoipata kwa malengo yaliyokusudiwa na sio vinginevyo.
Vilevile ameonya kutumia mikopo hiyo kwa mambo ya anasa na
kuongeza nyumba ndogo, badala yake waitumie kwa nidhamu pamoja na kuirejesha
kwa wakati.
Akizungumza katika mkutano huo, naye Mratibu wa mifuko ya
uwezeshaji toka baraza la taifa la uwezeshaji wananchi kiuchumi, Nyakao Mahemba
alifafanua kuwa vikundi hivyo vya DMI vimekidhi vigezo baada kufungua akaunti
katika benki ya Posta na kujiwekea akiba.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa vikundi hivyo mkoani Ruvuma,
Speciosa Katambala, amemuhakikishia mbunge huyo kuwa yale yote aliyowaagiza
watayafanyia kazi ikiwemo kuendelea kuhamasisha wananchi wilaya zote za mkoa
huo, kuendelea kujiunga na vikundi hivyo pamoja na kutumia mikopo watakayopata
kwa malengo yaliyokusudiwa.
No comments:
Post a Comment