Na Kassian Nyandindi,
KINYWAJI kama kahawa ni moja kati ya bidhaa muhimu
na maarufu inayopendwa duniani, vilevile ni chanzo cha mapato kwa nchi
zinazohusika na soko hilo, ambapo uzalishaji wa zao hili si kazi rahisi bali ni
kazi ngumu inayohitaji ujuzi wa hali ya juu.
Aidha katika kuwawezesha wakulima wa zao hilo, kuzalisha
kahawa kwa viwango vyenye ubora mara zote sekta husika wakiwemo maafisa kilimo
na ushirika ndiyo tunatambua wamepewa jukumu la kuwaelimisha wakulima hao, mara
kwa mara namna ya uzalishaji huo.
Wilaya ya Nyasa iliyopo mkoani Ruvuma, ni moja kati ya wilaya
ambayo wakulima wake wanazalisha kahawa ambapo jitihada mbalimbali
zimekuwa zikifanywa ili kuboresha uzalishaji wake, kwa kuwahimiza wakulima
wazingatie kanuni bora za kilimo cha zao hilo.
Katika kuhamasisha wakulima kujiunga kwenye vikundi au
ushirika, serikali siku zote imekuwa ikisisitiza jambo hili ikiwemo
uzalishaji wa mazao mbalimbali kwa pamoja ili kuongeza ufanisi na
muungano huo, ni rahisi wataalamu wa kilimo kuwafikia na kuwapa utaalamu husika
kuliko kumpitia mkulima mmoja mmoja.
Siku zote ili kuweza kuzalisha kahawa yenye ubora
wakulima wa zao hilo wilayani humo, wamejiwekea mikakati ya kuendelea
kuhamasishana na kujiunga kwenye vyama vya ushirika vya mazao ya chakula na
biashara.
Akihutubia katika mkutano mkuu wa ufunguzi wa msimu wa
ushirika kwa wanachama wa chama cha ushirika Luhangarasi kilichopo katika kata
ya Luhangarasi wilayani Nyasa, Afisa ushirika wa wilaya hiyo Menance Ndomba
anawataka wakulima wote wa mazao hayo ya chakula na biashara wajenge dhamira
kuu ya kujiunga pamoja ili waweze kuondokana na changamoto ya kufanya biashara
na makampuni binafsi, ambayo yamekuwa yakimnyonya mkulima na kumwacha aendelee
kubaki kuwa maskini.
Ndomba anasema kuwa wilaya hiyo ina vyama vya ushirika vitano
ambavyo ni Mapendo, Lipo, Kingirikiti, Nambawala pamoja na Luhangarasi ambapo
wakulima wanaounda ushirika kwenye vyama hivyo wameamua kujiunga kwa umoja wao
na kufungua msimu wa ukusanyaji wa kahawa bora, hatimaye kutafuta soko zuri
mnadani litakaloweza kuwafanya wauze kahawa yao na kupata faida kwa kila
mkulima atakayeuza kahawa yake huko.
Wanachama hao wa vyama hivyo vya ushirika walikutana Juni 11
mwaka huu katika kijiji cha Kimbango kata ya Luhangarasi wilayani hapa, kwa
lengo pia la kufungua mtambo wa kukobolea kahawa mbivu ya maganda ambayo
humenywa maganda yake, huoshwa na maji safi kisha kuanikwa kwenye vichanja
hatimaye kuwa katika viwango vinavyokubalika ili iweze kupata bei nzuri katika
soko la dunia.
“Ndugu zangu wakulima nasisitiza pelekeni kahawa zenu kwenye
vyama vya ushirika tuache kuuza kwa mtindo wa magoma kwa kubadilishana na
bidhaa fulani, tukifanya hivi hakika hatutaweza kunufaika na ushirika wetu”,
alisisitiza Ndomba.
Anasema kuwa siku zote wanunuzi binafsi wamekuwa na mbinu za
ujanja ambazo hudhoofisha maendeleo ya mkulima na kumwacha aendelee kubaki kuwa
maskini, hivyo wanapaswa kulitambua hilo na kukataa kuendelea kukandamizwa na
mtu yeyote kwani ushirika ni mahali salama ambapo pana mkono wa serikali ambao
humfanya mkulima kuwa salama na mali zake.
Vilevile aliwataka viongozi waliopo katika ushirika huo kuwa
waadilifu na mali za wanachama na kuwaelimisha wakulima wapeleke kahawa zao,
katika mitambo ya kuchakata kahawa mbivu ili iweze kuwa katika ubora na kupata
soko zuri.
Ofisa ushirika huyo wa wilaya ya Nyasa, Ndomba anabainisha
kuwa kupitia vyama vya ushirika mkulima amekuwa akinufaika kwa kupata huduma
kubwa za aina tatu ikiwemo mafunzo mbalimbali juu ya uendeshaji wa vyama hivyo,
kuwaunganisha na masoko ya nje, vyombo vya fedha pamoja na wagavi wa pembejeo
bora za kilimo.
Anaeleza kwamba mpango wa mafunzo husaidia kuboresha zao la
kahawa kutoka madaraja ya chini ya 10 hadi kufikia daraja la 4 ambapo haya
yote, hutokana na matokeo ya matumizi ya kusimika mashine za kati za kisasa
ambazo hukoboa kahawa mbivu kwa viwango vinavyokubalika.
Anafafanua zaidi kuwa mashine nyingi hutumia teknolojia ya
kisasa ambayo hutumia maji kidogo na kwamba, huondoa sukari kwenye punje ya
kahawa wakati wa kukoboa hivyo kutohitaji uvundikaji ambao hupunguza ubora
wake.
Anasema ujenzi wa vituo kwa ajili ya kufunga mashine hizi
kwenye vikundi unatekelezwa kwa mpango wa ushirikishwaji wa wakulima wenyewe
ambapo huchangishana fedha za kuinunua na kujengea banda la mashine, kuleta
maji safi kituoni, kujenga visima na mifereji, meza za kuanikia na ghala la
kuhifadhia kahawa.
Kuhusu mafunzo ya njia bora za kilimo cha kahawa kwa vikundi
husika vilivyosajiliwa kisheria, maafisa kilimo kwa kushirikiana na Taasisi ya
utafiti wa zao la kahawa (TACRI) wamekuwa bega kwa bega katika
kufanikisha azma hiyo.
“Pia wataalamu wa kilimo wamekuwa wakipitia taratibu za
uanzishwaji wa mashamba darasa kwa kila kikundi na kuweka ushindani kati yao,
ikiwa ni lengo la kuhamasisha waweze kuzalisha kahawa iliyobora na ambayo
itapata soko zuri”, anasema.
Kwa upande wake Katibu wa vyama vya ushirika wilaya ya Nyasa,
Batazary Hyera anaeleza kuwa ndani ya vyama hivyo vitano vya ushirika vilivyopo
wilayani humo wameweza kuanzisha pia vyama vya akiba na mikopo (SACCOS) ambavyo
vimesajiliwa kwa mujibu wa sheria ya ushirika wa vyama vya akiba na mikopo.
Anasema kwamba vyama hivyo, vimekuwa vikihudumia wanachama
wake ambao wenye hisa na wakulima wanaofikia idadi ya 8,663 kila mwaka katika
kanda zinazolima mazao ya chakula na biashara.
Hyera anaongeza kuwa wamekuwa wakitoa huduma nyingi za pembejeo
za kilimo, ikiwa ni lengo la kukuza na kuboresha mazao ya wakulima hususani kwa
kilimo cha zao la kahawa na mahindi katika kanda zinazoshughulika na mazao
hayo.
Katika msimu wa mwaka 2015/2016 anasema jumla ya mifuko 7,131
ya pembejeo za kilimo, wameweza kuwakopesha wanachama wao ili kuweza kuongeza
uzalishaji na kukuza kipato miongoni mwao.
Pia katika msimu huo walianzisha mfuko wa pembejeo
unaomilikiwa na vyama vyenyewe wilayani humo, wenye thamani ya shilingi milioni
33,685,450 ukiwa na malengo ya kupunguza mikopo ya pembejeo ili kumfanya
mkulima aweze kumudu gharama zake na kuboresha mazao shambani.
Akizungumzia mikakati waliyojiwekea ya ukusanyaji kahawa
Katibu huyo wa vyama vya ushirika wilayani hapa, Hyera anasema kuwa wamejiwekea
mikakati ya kukusanya kilo 808,450 za kahawa kwa msimu wa 2016/2017 sawa na
ongezeko la asilimia 20 ya makusanyo yaliyokusanywa na vyama hivyo, katika
msimu wa mwaka 2015/2016 ambapo yalikuwa kilo 673,709.
Sambamba na hilo, Hyera anaeleza kwamba katika kuboresha
ubora wa kahawa vyama hivyo vitano vya ushirika wilayani Nyasa, vitasambaziwa
pembejeo za kilimo yaani mbolea mifuko 10,000 katika msimu wa kuelekea kipindi
cha mvua 2016/2017 ili wakulima wake, waweze kuboresha mazao yao shambani.
Anaeleza kuwa vyama hivyo pia hivi sasa vinamiliki na
kuendesha mitambo 17 ya kuchakata kahawa mbivu, ambayo inaendelea kusimamiwa
vizuri na kufanikisha uzalishaji toka tani 249 msimu wa mwaka 2014/2015 hadi
tani 673 kwa mwaka 2015/2016.
Hyera anaongeza kuwa siku zote kwenye mafanikio hapakosi
changamoto, hivyo wanakabiliwa na tatizo la uwezo mdogo wa vyama kukabili
ushindani katika mfumo wa soko huria, kutokana na kuwa na mtaji mdogo wa kuweza
kuendeshea vyama hivyo.
Anasema changamoto kubwa nyingine inayowakabili ni uelewa
mdogo wa baadhi ya wakulima juu ya uzalishaji bora wa kahawa ambapo baadhi yao
wamekuwa na tabia ya kukoboa kahawa zao nyumbani, badala ya kupeleka kwenye
mitambo ya kisasa ya kukobolea zao hilo ambayo inamilikiwa na vyama vya
ushirika.
Pamoja na mambo mengine anasema, kuanzishwa kwa SACCOS katika
ushirika wao kutawawezesha wakulima kuepukana na wafanyabiashara walanguzi
ambao huzunguka vijijini na kuwarubuni wakulima, wakope fedha na mwisho wa siku
hutakiwa kulipa kahawa wakati wa mavuno.
Hata hivyo anatoa msisitizo kwamba wakati umefika kwa
wakulima wenzake kuachana na wafanyabiashara hao wajanja badala yake wajiunge
na vyama vya ushirika wilaya ya Nyasa, ili waweze kufaidika pia na mafunzo
yanayotolewa kuhusiana na suala zima la uzalishaji wa kahawa bora hatimaye
wazalishe kwa wingi na yenye ubora unaokubalika katika soko la kimataifa.
Mwandishi wa makala haya ni mchambuzi pia wa makala za uchunguzi na habari za aina mbalimbali anapatikana kwa simu namba 0762 578960 au barua pepe; nyandindi2006@yahoo.com
No comments:
Post a Comment