Na Muhidin Amri,
Mbinga.
WILAYA ya Mbinga mkoani Ruvuma, kupitia halmashauri zake mbili
ya mji wa Mbinga na wilaya hiyo, imefanikiwa kukamilisha mradi wa
utengenezaji madawati kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la upungufu uliopo katika
shule za msingi na sekondari wilayani humo.
Kazi hiyo imefuatia utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. John
Magufuli kwa Wakurugenzi, Wakuu wa wilaya na mikoa hapa nchini kuhakikisha kwamba
wanatumia rasimali za misitu iliyopo katika maeneo yao, ili kumaliza
tatizo hilo la uhaba wa madawati na kuwafanya watoto waliopo shuleni kushindwa
kufanya vizuri katika masomo yao kutokana na kukosa madawati ya kukalia
wanapokuwa darasani.
Mkurugenzi mtendaji wa Hamashauri ya wilaya ya Mbinga,
Venance Mwamengo alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu
ambapo alifafanua kwamba wilaya hiyo, ilikuwa na upungufu wa madawati 12,952
kati ya hayo kwa shule za msingi ni 8,452 na kwa shule za sekondari upungufu wa
viti na meza ulikuwa 4,500.
Alifafanua kuwa hadi kufikia Juni 30 mwaka huu ambao ni muda
wa mwisho wa utekelezaji wa agizo hilo, tayari Halmashauri yake ilifanikiwa
kutengeneza madawati 8,000 hivyo kubakia madawati 4,50 ambayo wanatarajia
kukamilisha ndani ya siku chache zijazo kutokana na vifaa vyote muhimu
kama vile nondo na mbao vipo tayari kwa ajili ya kukamilisha kazi hiyo.
Pia Mwamengo alisema kwa shule za sekondari
wamekamilisha kazi hiyo na kubakiwa na ziada ya viti na meza 1,000 ambazo
zitasambazwa katika shule za msingi, zinazokabiliwa na upungufu huo
kwa lengo la kumaliza kabisa tatizo hilo la madawati katika wilaya hiyo.
“Hapa tayari tumefanikisha kumaliza kazi ya kutengeneza viti
na meza kwa shule za sekondari na sasa tunaendelea kumalizia kuunganisha
madawati yaliyobakia kwa shule za msingi ambapo ndani ya siku chache, tutakuwa
tumeshamaliza zoezi hili”, alisema.
Kwa mujibu wa Mwamengo ni kwamba wilaya ya Mbinga,
ilitenga kiasi cha shillingi milioni 475,820 kwa ajili ya
kukabiliana na upungufu wa madawati, meza na viti kwa shule za msingi na
sekondari.
Alifafanua kuwa kiasi hicho cha fedha ni gharama za kununulia
mashine za kuranda, kukata na kukunja vyuma, mashine za kupasulia mbao, umeme
na gharama zingine ndogo ndogo ambapo vyote kwa ujumla vimetengenezwa kwa kutumia
mbao pamoja na chuma ili kufanya viweze kuwa imara zaidi, ikilinganishwa na
madawati yanayotengenezwa kwa mbao tupu ambayo huharibika haraka.
No comments:
Post a Comment