Mkuu wa wilaya ya Namtumbo mkoani humo, Chande Nalicho akisisitiza jambo kwa kuwataka wananchi wa wilaya hiyo kuacha kuharibu vyanzo vya maji, ikiwemo suala la ukataji miti na uchomaji misitu hovyo. |
Na Kassian Nyandindi,
Namtumbo.
MKUU wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Chande Nalicho
ametoa agizo kwa kuitaka mamlaka husika wilayani humo kuwachukulia hatua za
kisheria watu waliovamia vyanzo vya maji, kutokana na wilaya hiyo hivi sasa
kukabiliwa na tatizo kubwa la upatikanaji wa maji safi na salama.
Aidha ameagiza pia waharibifu hao wa mazingira, wanapaswa
kufikishwa Mahakamani ili iweze kuwa fundisho kwa wengine wenye tabia ya
kuharibu mazingira, ikiwemo ukataji wa miti hovyo.
Tumaini Mgaya Ofisa maendeleo ya jamii Namtumbo, akisisitiza jambo kwenye mafunzo hayo. |
Nalicho alisema kuwa tangu enzi za mababu zetu walikuwa
wakikemea tabia hii ya uharibifu wa mazingira, hivyo kuna kila sababu kwa jamii
kurithi tabia hiyo ili kuweza kuepukana na tatizo la mabadiliko ya tabia nchi,
ambalo linahatarisha usalama wa maendeleo ya viumbe hai hapa duniani.
Agizo hilo la Mkuu huyo wa wilaya ya Namtumbo, Nalicho
lilitolewa juzi alipokuwa akifungua mdahalo wa athari na changamoto za
mabadiliko ya tabia nchi kwa wanawake wa wilaya hiyo, uliofanyika ukumbi wa
Bikira Maria wa Fatima, mjini hapa.
“Nimetoa maelekezo kwa watalaamu wangu wa wilaya, kamateni
waharibifu wote wa mazingira pelekeni mahakamani wakalipe faini au wafungwe
jela na wale wanaolima katika vyanzo vya maji watoke haraka, kabla dola
haijachukua jukumu la kuwatoa kwa kutumia nguvu”, alisisitiza Nalicho.
Vilevile alisema kuwa athari za mabadiliko ya tabia nchi
zinapotokea, wanaohangaika na kuteseka ni wanawake na watoto wadogo hivyo
ameitaka jamii wilayani humo, kujenga ushirikiano ili waweze kukabiliana na
hali hiyo na kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Kadhalika alifafanua kuwa endapo wananchi wasipozingatia
maelekezo yanayotolewa na serikali, kuna hatari ya kuiweka nchi yetu katika
mazingira mabaya na kubaki kuwa maskini huku akiongeza kuwa hata tabia ya
uchomaji moto misitu hovyo katika wilaya ya Namtumbo, wananchi wanapaswa
kuiacha mara moja.
Awali kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa shirika lisilokuwa
la kiserikali hapa nchini la Mbarali Water Sanitation and Environmental
Conservation Organisation (MWECO), Terdey Mhagama alifafanua kuwa mdahalo huo
umeshirikisha baadhi ya wanawake 70 wa
kutoka wilaya ya Namtumbo kwa lengo la kujenga uwezo katika masuala ya kiuchumi
kwa jamii na kufanya utetezi katika upatikanaji wa rasilimali za maji, uhifadhi
wa vyanzo vya maji na mazingira.
Mhagama alieleza kuwa tafiti zinaonesha kwamba ndani ya miaka
20 ijayo ukanda wa Afrika ya kati, mashariki na kusini, Tanzania ikiwa mojawapo
zitakuwa jangwa kabisa kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira unaoendelea
kufanyika katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Alisema hali hii inabainisha kwamba ukame utakuwa umetokea
kila mahali, mafuriko wakati wa mvua yataathiri makazi ya watu na hakutakuwepo
miti ya kunyonya maji ya mvua chini ya ardhi, ili jamii isiweze kuathirika.
Hivyo wananchi wa wilaya ya Namtumbo, wamesisitizwa kutunza
mazingira kwa kila hali ili waweze kuishi maisha mazuri na kwamba endapo kama
watakuwa wamefanikiwa katika hili, watakuwa wamejenga historia kwa faida ya
kizazi cha sasa na kijacho.
No comments:
Post a Comment