Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
KATIKA kuhakikisha kwamba, Halmashauri ya wilaya ya Mbinga
mkoani Ruvuma inadhibiti vyanzo vyake vya mapato kupitia vituo vya kukusanyia
ushuru wa mazao, hivi sasa imenunua mashine za Kieletroniki (EFD’S) ambazo
zitatumika kwa ajili ya kufanya kazi hiyo.
Ujenzi wa jumla ya vituo 13 vya kukusanyia ushuru huo
vilivyopo wilayani humo, vitafungwa mashine hizo ambapo jumla ya shilingi
milioni 400,000,000 kutoka mapato ya ndani ya halmashauri hiyo, zitatumika
katika kukamilisha kazi ya ujenzi wa vituo hivyo na kufungwa mashine za EFD’S.
Hayo yalisemwa juzi na Mweka hazina wa wilaya ya Mbinga,
Joseph Mazito wakati alipokuwa akisoma taarifa ya uzinduzi wa kituo cha
kukusanyia ushuru wa mazao kilichopo kijiji cha Kihulila wilayani humo, kwa
kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, George Mbijima.
Mazito alifafanua kuwa lengo la kufanya hivyo ni kutimiza
agizo la serikali la ukusanyaji mapato kwa mfumo wa kieletroniki, kuanzia mwezi
Julai mwaka huu na kutoa elimu kwa wananchi wa wilaya hiyo waweze kulipa ushuru
na kodi mbalimbali kwa wakati.
Alisema kuwa kufungwa kwa mashine hizo, kutarahisisha huduma
za malipo ya mapato kufanyika kwa wakati na kuweza kuokoa muda wa kufanya
shughuli nyingine za maendeleo ya wananchi.
Alieleza kuwa, mfumo huo wa EFD’S utaweza kuongeza ukusanyaji
wa mapato ya ndani ya halmashauri na kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato
hayo.
Hata hivyo kwa upande wake kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru
kitaifa Mbijima, alipongeza jitihada hizo zinazofanywa na halmashauri hiyo kwa
kudhibiti mapato hayo huku akiutaka uongozi husika kuhakikisha kwamba, kazi
hiyo inafanywa kikamilifu na kuwa endelevu kwa manufaa ya jamii kwa kuelekeza
fedha hizo zinazopatikana kupitia makusanyo hayo kwenda kutekeleza miradi ya
maendeleo ya wananchi.
No comments:
Post a Comment