Na Muhidin Amri,
Mbinga.
WAKULIMA katika kata ya Litumbandyosi wilayani Mbinga mkoa wa
Ruvuma, wameiomba serikali kuandaa sheria kali itakayowabana wafanyabiashara
kuacha tabia ya kununua mazao ya wakulima, kwa kutumia vipimo haramu (lumbesa)
ambapo hununua kwa bei ndogo isiyolingana na gharama ya uzalishaji.
Senyi Ngaga. |
Wakulima hao walisema hayo kwa nyakati tofauti, wakidai kuwa wafanyabiashara
hao wamekuwa na tabia ya kwenda vijijini hasa mashambani na kutumia vipimo visivyokubalika
kisheria kama vile bakuri na ndoo, kwa ajili ya kununua mazao kama vile
mpunga na mahindi jambo ambalo huchangia kuwanyonya wakulima na kuwaacha maskini,
licha ya kazi kubwa wanayofanya kila mwaka.
Aidha walieleza kuwa kutokana na kuwa na hali ngumu ya maisha
ikiwemo suala la upatikanaji wa masoko, wamekuwa wakati mwingine wakilazimika
kuuza mazao yao kwa mtindo huo wa vipimo wanavyotumia walanguzi hao ili waweze
kujikimu kimaisha ikiwemo suala la kupeleka watoto wao shule.
Theresia Kinyeru ambaye ni mkulima wa zao la mpunga katika
kijiji cha Mabuni kata ya Litumbandyosi, alisema wamekuwa wakiteseka na hali
hiyo kwa muda mrefu lakini wanashindwa kudhibiti kutokana na wasimamizi wa
sheria za vipimo wamekuwa wakikaa mjini, badala ya kwenda vijijini ambako
vitendo vingi vya dhuluma vimekuwa vikifanyika.
Alisema wamekuwa wakipata taabu kuanzia hatua ya awali ya
maandalizi ya mashamba yao hadi kufikia uvunaji lakini wajanja wachache
wasiokuwa na huruma na mkulima, hutumia mbinu za ujanja kuwanyonya nguvu
zao kwa kununua mazao yao kwa bei ndogo.
Kinyeru ameitaka serikali kuwaongeza maafisa vipimo hadi
ngazi ya kata, ambao watafanya kazi vijijini hasa pale kipindi cha msimu
wa mavuno ya mazao yao shambani, ili waweze kusimamia vizuri suala hilo kwa
ufanisi mzuri.
Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga, kwa upande wake amewaagiza
watendaji wa vijiji na kata kuhakikisha kwamba wanasimamia vyema suala la
uuzaji na ununuzi wa mazao ya mkulima ikiwemo kudhibiti wafanyabiashara
wanaotumia vipimo visivyokubalika na ambavyo humnyonya mkulima na kumfanya
aendelee kuwa maskini.
Ngaga pia alipiga marufuku wafanyabiashara kwenda mashambani
kununua mazao ya mkulima, badala yake watumie vituo maalum kama vile maeneo ya
siku ya minada ambayo yametengwa kwa ajili ya kazi hiyo, pamoja na kutumia
vipimo halisi kama vile mizani zilizopimwa kisheria.
“Nilikwisha waagiza watendaji wangu wote kusimamia jambo
hili, tuna upungufu mkubwa wa maafisa vipimo katika wilaya yetu ya Mbinga sasa
nimetoa mwongozo watendaji wa vijiji na kata ndiyo watakuwa wasimamizi wa kazi
hii, lengo hapa nataka kila mmoja awajibike katika kuchangia uchumi
wa nchi yetu”, alisema Ngaga.
No comments:
Post a Comment