Na Steven Augustino,
Tunduru.
WAUMINI wa dhehebu la Roman Katoliki, kutoka Jimbo la
Tunduru – Masasi mkoani Ruvuma wamepangwa kushiriki kongamano la kitaifa la Ekaristi
takatifu na utoto mtakatifu, ambalo limepangwa kufanyika mkoani Mwanza Juni
Mosi mwaka huu.
Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa kamati ya Kongamano hilo,
Chrispin Mumba alipokuwa kwenye mahojiano maalumu, yaliyofanyika na mwandishi
wetu katika ofisi za jimbo hilo.
Mumba alisema kuwa katika msafara huo kutakuwa na watoto wa
Kipapa, mapadre na walei kutoka Parokia mbalimbali za Jimbo la Tunduru - Masasi.
Alisema waumini hao wanatarajia kuanza safari yao Juni 6 na
kupokelewa mkoani Mwanza Juni 8 mwaka huu, tayari kwa kushiriki sherehe hizo
ambazo zimepangwa kuishia Juni 12 mwaka huu.
Akizungumzia safari ya maadhimisho hayo, naye Makamu Askofu
wa Jimbo hilo Padri Jordan Liviga alisema kuwa jimbo lake ambalo lilikuwa
mwenyeji wa sherehe za utoto mtakatifu, zilizofanyika kitaifa wilayani
Tunduru mkoani Ruvuma mwaka 2014, pamoja na mambo mengine watoto hao
wanatarajia kwenda kukabidhi msalaba katika Jimbo Katoliki la Mwanza.
Padri Liviga alifafanua kwamba, waumini na watoto hao
wamepatikana na kupatiwa baraka na waumini wa dhehebu hilo kutoka katika
Parokia mbalimbali za jimbo la Tunduru – Masasi.
No comments:
Post a Comment