Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
JENGO la utawala ambalo hutumika na Walimu wa shule ya
sekondari Kitura katika kata ya Kitura wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, lina
hali mbaya ambapo wakati wowote huenda likabomoka na kuleta madhara kwa
watumiaji.
Miundo mbinu ya jengo hilo ambayo ni chakavu na imetengeneza
nyufa, hivi sasa baadhi ya kuta zake zimeanza kubomoka na kuhatarisha usalama
wa walimu wanaofundisha katika shule hiyo.
Wakizungumza na waandishi wa habari ambao walitembelea shuleni
hapo huku wakiomba majina yao yasitajwe gazetini, walimu hao walisema kuwa hata
mazingira ya shule yao yamekuwa magumu ambapo vyoo vya wanafunzi na nyumba za
walimu zilizopo hazikidhi mahitaji husika.
Kadhalika walieleza kuwa kuna kila sababu kwa uongozi husika
kuchukua hatua za haraka kunusuru hali hiyo, ili isiweze kuleta madhara makubwa
hapo baadaye na kuwafanya walimu wakate tamaa ya kuendelea kufundisha katika
shule hiyo.
Diwani wa kata ya Kitura Alex Ngui alipoulizwa juu ya tatizo
hilo, alikiri kuwepo kwa matatizo hayo na kufafanua kuwa hivi sasa wameweka
mikakati ya kuhamasisha wananchi wake kufyatua tofari ambazo zitasaidia kuanza
kazi ya ujenzi wa jengo hilo la utawala katika shule ya sekondari Kitura,
pamoja na vyoo na nyumba za walimu.
Alisema wananchi walikuwa wanashindwa kuanza kuchangia nguvu
zao ikiwemo ufyatuaji wa tofari za udongo, kutokana na mvua za masika ambazo
zilikuwa zikinyesha mara kwa mara hivyo walikuwa wakisubiri ziishe ndipo waanze
kufanya kazi hiyo.
Ngui alifafanua kuwa kupitia vikao vyake vya kata ambavyo
amekuwa akivifanya, wamejiwekea malengo pia ya kuushirikisha uongozi wa
Halmashauri ya wilaya hiyo uweze kusaidia vifaa vya kiwandani mara baada ya
wananchi kuchangia nguvu zao, kama vile mchanga, mbao na ufyatuaji wa tofari za
udongo.
Hata hivyo alisema kuwa, pia wameweza kuibua mradi wa madaraja
mawili kutoka kijiji cha Mahilo kwenda makao makuu ya kata hiyo ambapo
utekelezaji wake utaanza katika bajeti ya maendeleo ya wilaya ya Mbinga, kwa
mwaka wa fedha wa 2016/2017 madaraja hayo ujenzi wake utakuwa umekamilika.
No comments:
Post a Comment