Na Steven Augustino,
Tunduru.
MKUU wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Agnes Hokororo
amewataka wafanya biashara na wadau wengine wa maendeleo wilayani humo kujitokeza
na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali katika kusaidia ujenzi na
ukarabati wa miundombinu ya shule za wilaya hiyo, ambazo zimekuwa chakavu kwa
lengo la kuboresha mazingira ya kusomea wanafunzi.
Hokororo alitoa wito huo juzi, alipokuwa akipokea msaada wa
shilingi milioni 2.5 kutoka kwa Meneja wa sheria na usuluhishi wa kampuni ya
Export Trading Group (ETG) Nasser Mansour, katika hafla fupi iliyofanyika katika
kiwanda cha kubangua Korosho kinachofahamika kwa jina la Korosho Afrika Limited
kilichopo mjini hapa.
Alisema kuwa fedha hizo zimetolewa kwa wakati muafaka huku
akiahidi kuzisimamia kikamilifu kwa kuhakikisha kwamba, zinatumika kwa ajili ya
kufanyia kazi iliyolengwa.
Kadhalika akitoa maelezo mafupi juu ya msaada huo, Meneja Mansour
alimweleza Mkuu wa wilaya hiyo, Hokororo kuwa msaada huo ni sehemu ya faida
ambayo kampuni imejipangia kurejesha kwa njia ya kutoa huduma kwa jamii na kwamba,
zitafanya kazi ya kufanya ukarabati wa madarasa na kutengeneza madawati katika
shule ya msingi majengo iliyopo mjini Tunduru.
Vilevile akitoa taarifa ya utekelezaji wa kiwanda hicho, Meneja
wa kampuni hiyo ya (ETG) Vinesh Mathew alifafanua kuwa kiwanda hicho kilianza
shughuli za ubanguaji korosho wilayani humo, mapema mwanzoni mwa mwezi Aprili mwaka
2008 ambapo kimekuwa ni tegemeo la kutoa ajira kwa wakazi wa wilaya hiyo.
Kwa mujibu wa takwimu kutoka ndani ya uongozi wa kiwanda hicho,
zinaeleza kuwa jumla ya watu 700 wanawake na wanaume wamekuwa wakinufaika kwa
kupewa ajira katika eneo la kiwanda, wakati wa msimu wa mavuno ya korosho na
shughuli za ubanguaji zinapofanyika.
Pia watu hao huishi kwa kutegemea ajira za muda, lakini
hunufaika kutokana na kipato wanachokipata wao na familia zao zinazowazunguka
katika kujiletea maendeleo.
Shughuli zinazofanywa katika kiwanda hicho ni pamoja na
ununuzi wa korosho, ukaushaji, ubanguaji, upangaji kwa madaraja husika,
upakiaji na uuzaji wa zao hilo katika masoko yaliyopo nje ya nchi.
No comments:
Post a Comment