Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
SENYI Ngaga ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, amewataka
Madiwani wa Halmashauri ya wilaya hiyo kusimamia kikamilifu na kuwa wakali juu
ya matumizi ya fedha zinazotolewa na serikali, ili ziweze kufanya kazi husika
na kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Agizo hilo lilitolewa na Mkuu huyo wa wilaya, Ngaga alipokuwa
akizungumza na Madiwani hao kwenye kikao maalumu cha kujadili taarifa ya Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ((CAG) kwa mwaka fedha unaoishia Juni 30
mwaka 2015, ambapo Halmashauri ya Mbinga imepata hati yenye mashaka.
Senyi Ngaga, Mkuu wa wilaya ya Mbinga. |
Ngaga alisema hayo kufuatia mapungufu na hoja mbalimbali
zilizotolewa na CAG kwa Halmashauri hiyo, kufuatia kuwepo kwa matumizi ya fedha
yasiyofuata miongozo na taratibu husika.
“Hoja hizi zilizotolewa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu
za Serikali ndugu zangu Madiwani zinapaswa kufanyiwa kazi mapema, vilevile muwe
wakali juu ya matumizi na manunuzi ya fedha za serikali”, alisema Ngaga.
Alisema kuwa hategemei tena kuona mapungufu yaliyojitokeza
katika mwaka huo yanajirudia tena kwa mwaka 2016/2017 na kwamba aliwataka
kutumia nafasi zao za udiwani kutekeleza majukumu ya wananchi ipasavyo.
“Huu ni uzembe hatutegemei mambo haya yajirudie tena, tusiachane
twendeni pamoja ili tuweze kujenga wilaya yetu iweze kusonga mbele kwa
kutekeleza majukumu haya ya wananchi kwa kufuata taratibu na miongozo husika”,
alisisitiza.
Pamoja na mambo mengine, awali Madiwani hao walisema kuwa
wanaiomba serikali kuwachukulia hatua watendaji wa Halmashauri ya wilaya ya
Mbinga, ambao walihusika kwa namna moja au nyingine kushindwa kutekeleza
majukumu husika ikiwemo kutofunga hesabu za halmashauri ya wilaya hiyo, kwa wakati.
Madiwani hao walishangazwa pia na kutokuwepo kwa mfumo mzuri
wa utunzaji wa daftari la mali za kudumu, halmashauri kuwa na madeni yaliyodumu
kwa muda mrefu bila walengwa husika kulipwa, magari yaliyochakaa kuuzwa bila
kufuata miongozo husika, udhibiti wa ndani wa fedha na utendaji kazi wa bodi ya
zabuni usioridhisha ambao wamekuwa wakifanya malipo na manunuzi bila kufuata
sheria za manunuzi.
Hata hivyo waliongeza kuwa watendaji wa namna hiyo, ambao
wanaonesha kufanya kazi kwa mazoea sheria inapaswa kuchukua mkondo wake dhidi
yao ili kudhibiti hali hiyo isiweze kuendelea.
No comments:
Post a Comment