Na Muhidin Amri,
Mbinga.
WANANCHI mkoani Ruvuma, wamehimizwa kuwa na tabia ya kutunza
miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na serikali kwa fedha nyingi, yenye
lengo la kuharakisha kukua kwa uchumi wa mkoa huo na taifa kwa jumla.
Aidha wametakiwa kuacha kuhujumu miradi hiyo, ili kuepusha
uwezekanao wa kukatisha tamaa baadhi ya wahisani ambao wanajitolea fedha
zao nyingi kujenga miundombinu husika, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi
za serikali katika kukabiliana na changamoto zilizopo hasa katika utoaji wa huduma
muhimu za kijamii.
Wito huo umetolewa juzi na kiongozi wa mbio za Mwenge wa
uhuru kitaifa George Mbijima, alipokuwa akifungua zahanati ya kijiji cha
Kihulila wilayani Mbinga ambayo ilijengwa kwa fedha za mapato ya
ndani ya halmashauri ya wilaya hiyo, ili kuwaondolea kero wakazi wa kijiji
hicho na maeneo ya jirani kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya.
Mbijima alisema kuwa siku zote serikali ndiyo inayotoa
fedha za kukamilisha ujenzi wa mradi wowote ule, huku akisema kuwa hata
zahanati hiyo ambayo ilianza kujengwa mwaka 2008 kuna kila sababu kwa wananchi
kuitunza ili iwe endelevu na kusaidia katika suala zima la kuharakisha
maendeleo katika maeneo yao.
Alisema kuwa licha ya serikali kutumia fedha nyingi
kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo lakini bado kuna fikra potofu,
iliyojengeka miongoni mwa watu wachache hapa nchini kwamba kila jambo
linalofanywa na serikali wananchi hawapaswi kuitunza au kuunga mkono kitendo
ambacho kiongozi huyo wa mbio za mwenge alikemea na kuitaka jamii kuachana na hali
hiyo.
Kwa mujibu wa Mbijima alieleza kwamba, kuhujumu miradi hiyo
ni sawa na kujiua wenyewe kwa sababu inatekelezwa kwa kutumia kodi za
wananchi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadae.
No comments:
Post a Comment