Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.
BAADHI ya Wananchi wa kijiji cha Kihuru na Nkaya katika kata
ya Lituhi wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, wameilalamikia Ofisi ya Mkuu wa wilaya
hiyo kwa kushindwa kusimamia ipasavyo ugawaji wa chakula cha msaada ambacho kimetolewa
na serikali kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa vijiji hivyo, ambao walikumbwa
na maafa ya kuzolewa nyumba na mazao yao shambani.
Rais Dkt. John Magufuli. |
Maafa hayo ambayo yalitokea Aprili 4 hadi 8 mwaka huu,
kufuatia mvua kubwa iliyonyesha siku nne mfululizo ambayo iliambatana na upepo
mkali ambapo zaidi ya wananchi 1,000 walikosa mahali pa kuishi, kufuatia nyumba
na mazao yao waliyolima shambani kuzolewa na mkondo mkubwa wa mafuriko ya maji
ambao ulikuwa ukielekea ziwa Nyasa wilayani humo.
Wakizungumza kwa kuomba majina yao yasitajwe kwenye mtandao huu, walisema kuwa wameshangazwa na Ofisi hiyo ya Mkuu wa wilaya kutosimamia kwa karibu zoezi hilo la ugawaji wa mahindi hayo
ambayo yametolewa na serikali tarehe 18 mwezi Mei mwaka huu, ili yaweze
kuwasaidia wahanga hao ambao wamekumbwa na mkasa huo.
Aidha walieleza kwamba taarifa juu ya malalamiko hayo, Mkuu
wa wilaya ya Nyasa, Margaret Malenga yamemfikia lakini hawaoni jitihada
zinazoendelea kufanyika katika kunusuru hali hiyo, hivyo wanauomba uongozi wa
ngazi ya juu serikalini uingilie kati na kuweza kupata haki yao ya msingi.
Vilevile kufuatia hali hiyo walisema wamekosa imani na Afisa
mtendaji wa kata hiyo, Charles Chikuni na Diwani wake Dominick Mahundi ambapo licha
ya viongozi hao wa kata hiyo ya Lituhi kupewa dhamana ya kusimamia zoezi la ugawaji
wa mahindi hayo kwa kufuata taratibu husika, wameshindwa kutekeleza ipasavyo
badala yake wamekuwa wakiyagawa kwa upendeleo hata kwa watu wengine ambao hawahusiki
katika zoezi hilo.
“Sisi inatusikitisha sana mahindi haya tokea yameletwa hapa
Lituhi yana wiki tatu sasa zimepita, viongozi wetu hawa wa kata wamekuwa wabinafsi
wanayagawa kwa kujuana na sio kwa kufuata utaratibu uliowekwa kulingana na
mahitaji ya walengwa walioathirika na maafa haya”, walisema.
Jumla ya tani 43.2 za mahindi ndizo ambazo serikali ilipeleka
kwa wahanga hao wa mafuriko katika kata ya Lituhi, ambapo ofisi inayosimamia masuala ya maafa hayo
yaliyotokea katika vijiji hivyo ni ya Mkuu wa wilaya hiyo.
Pamoja na mambo mengine, mwandishi wa habari hizi alipofanya
mahojiano na Afisa mtendaji wa kata hiyo, Chikuni alisema yeye malalamiko hayo
hayajamfikia ofisini kwake na hawezi kuzungumzia lolote.
“Naomba nikueleze sina malalamiko yoyote kwenye ofisi yangu
yaliyoletwa na wananchi hawa kuhusiana na mahindi haya ya msaada uliotolewa na
serikali, kwanza nakushangaa kwa nini uje unihoji mimi badala ya kwenda
kuwahoji waliokuletea taarifa hizi”, alisema Chikuni.
Pia Diwani wa kata ya Lituhi, Mahundi naye alipotakiwa
kutolea ufafanuzi juu ya malalamiko haya alisema, “mimi wahanga wa maafa haya
siwatambui, kama walikuja kwako siwezi kukueleza lolote juu ya taarifa zao kwa
sababu siwatambui”.
Hata hivyo alipotafutwa Mkuu wa wilaya ya Nyasa, Malenga
aweze kutolea ufafanuzi juu ya shutuma hizo hakuweza kupatikana ofisini kwake
na simu yake ilipopigwa ilipokelewa na alipoulizwa juu ya malalamiko hayo ya
wananchi wake, hakujibu lolote na badala yake aliishia kuikata na kwamba licha
ya jitihada ya kupiga tena mara kwa mara haikupokelewa.
No comments:
Post a Comment