Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, George Mbijima
amefungua mradi wa Hoteli ya kisasa iliyopo Mbinga mjini mkoani Ruvuma kwa
lengo la kukabiliana na uhaba wa hoteli unaoukabili mji huo, yenye thamani ya
shilingi milioni 110,000,000.
Akisoma taarifa ya mradi huo mbele ya Kiongozi wa mbio hizo
za Mwenge, Mary Thomas ambaye ni msimamizi wa mradi huo alisema kuwa mradi huo
ambao ni kitega uchumi yaani, “Kusile Restaurant and Lodge” ulibuniwa baada ya
kuona mji huo, una tatizo la upatikanaji wa hoteli ya kisasa.
Mary alifafanua kuwa kufunguliwa kwa jengo hilo ni kuunga
mkono jitihada za kimaendeleo zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano
inayoongozwa na Rais shupavu, John Magufuli katika kutengeneza ajira kwa vijana
wa Mbinga na Watanzania wote kwa ujumla ili kuweza kuongeza kipato na kukuza uchumi.
“Ndugu kiongozi wa mbio hizi za Mwenge wa Uhuru, mradi huu
umefanikiwa pia kuwawezesha wakulima wadogo wadogo 10 kuanzisha kilimo cha
mboga mboga maalumu ambazo hazipatikani hapa Mbinga, hivyo kutengeneza soko la
uhakika kwa mboga mboga hizo na zile za kawaida”, alisema Mary.
Pamoja na mambo mengine, alibainisha kuwa katika kutekeleza
azma hiyo Kusile hoteli imefanikiwa kutengeneza ajira 22 ambapo kati ya hizo
wanawake wapo 16 na wanaume sita.
Kwa upande wake Kiongozi huyo wa mbio za Mwenge, Mbijima
aliwataka watoa huduma katika hoteli hiyo wahakikishe kwamba wanatoa huduma
zinazolingana na hadhi ya jengo hilo, ili biashara wanazozifanya ziweze kuwa
endelevu.
Hata hivyo Mbijima amewapongeza wamiliki wa jengo hilo la
biashara, kwa ubunifu walioufanya ambao utasaidia kupunguza uhaba wa nyumba ya
kisasa ya kulala wageni na kuweza kupata huduma bora ya chakula.
No comments:
Post a Comment