Thursday, June 2, 2016

SHULE YA MSINGI NGAPA TUNDURU WALIMU NA WANAFUNZI WAJISAIDIA PORINI



Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako.


Na Steven Augustino,

Tunduru.

WANAFUNZI na walimu wa shule ya msingi Ngapa katika kata ya Ngapa wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wanajisaidia porini  kwa miaka miwili mfululizo sasa kufuatia shule hiyo kutokuwa na vyoo safi na salama, ambavyo vitawawezesha kwa ajili ya matumizi husika na utunzaji wa mazingira katika hali ya usafi kuzunguka shule hiyo.

Kufuatia hali hiyo shule hiyo yenye zaidi ya wanafunzi 589 wanaosoma hapo, wanaishi katika hatari ya kupata maambukizi ya magonjwa ya mlipuko kama vile homa za matumbo.

Vilevile walimu na wanafunzi hao wamekuwa wakiweka rehani maisha yao,  huenda wakashambuliwa na wanyama wakali wakiwemo chui, simba, fisi, mbweha na nyoka ambao hupatikana katika msitu uliopo jirani na shule hiyo wa kijiji cha Ngaga pale wanapoenda kujisaidia msituni humo.


Pia hali hiyo inasababishwa kutokana na baadhi ya vyoo vya shule hiyo, kubomolewa na mvua za masika zilizokuwa zimeambatana na upepo mkali mwezi February mwaka 2014.

Taarifa zinaeleza kuwa sambamba na kubomolewa kwa vyoo hivyo, pia mvua hizo zilibomoa madarasa manne kati ya madarasa saba yaliyokuwa yakitumika na wanafunzi kusomea, jambo ambalo hivi sasa linasababisha wanafunzi hao kusoma kwa kupeana zamu kwenye baadhi ya vyumba vya madarasa ambavyo havikubomolewa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wazazi na walezi wa watoto hao walisema kuwa kinachowashangaza tangu wakati huo hawajawahi kuuona uongozi husika ngazi ya wilaya kutembelea shuleni hapo, kwa lengo la kwenda kukaa pamoja na kutafuta suluhisho juu ya tatizo hilo.

Mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho, Ally Lionga alithibitisha uwepo wa hali hiyo na akatumia nafasi hiyo kuiomba serikali kupitia Waziri mwenye dhamana na masuala ya elimu kuingilia kati na kuhakikisha madarasa na vyoo hivyo vya shule ya msingi Ngapa, vinajengwa haraka ili kuwawezesha watoto hao kusoma katika mazingira mazuri.

Mwalimu Mkuu shule hiyo Christopher Mnipa alisema changamoto hiyo imekuwa ikiwatesa kwa muda mrefu sasa, ingawa shule yake imekuwa ikifanya vizuri katika matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya darasa la saba.

Diwani wa kata ya Ngapa Said Pindu alisema kuwa licha ya kulifikisha suala hilo katika vikao mbalimbali vya Halmashauri ya wilaya ya Tunduru, hajaona juhudi zozote zinazofanywa na uongozi husika.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Tina Sekambo alikiri kuwa na taarifa za kubomoka kwa vyoo na madarasa ya shule hiyo na kwamba alieleza kuwa kinachokwamisha kufanyika kwa ujenzi wa vyoo na madarasa hayo, hutokana na wazazi na wananchi wa kijiji hicho kugoma kujitolea kuchangia nguvu zao.

Sekambo alisema Halmashauri yake, kwa kuwashirikisha wataalamu  pamoja na Diwani  wa kata hiyo wanajipanga kwenda kutoa elimu na hamasa kwa wananchi hao kujitokeza kujitolea nguvu zao na serikali, iweze kuchangia vifaa vya kiwandani ili kuweza kumaliza kero hiyo.

No comments: