Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
VIJANA wanaojishughulisha na kazi ya ufyatuaji tofari za
udongo katika mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, wameshauriwa kujiunga na Kampuni ya
Ovans Construction Limited ili waweze kufanya kazi hiyo kwa kutumia mashine ya
kisasa ya kufyatua tofari za kuchanganya mchanga na simenti, ikiwa ni lengo la kuepukana
na uharibifu wa mazingira katika mji huo.
Uhamasishaji huo wa vijana kuachana na kazi ya ufyatuaji wa
tofari za udongo ambao hufanywa mabondeni, ni njia ya kuepukana pia na
uharibifu wa vyanzo vya maji ambao unaendelea kushika kasi kila siku katika mji
huo.
Valence Urio. |
Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Valence Urio alisema hayo juzi
alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake ambapo alifafanua
kuwa kazi hiyo ya uundaji wa tofari za udongo pia huchangia kwa kiasi kikubwa
uharibifu wa misitu, ambapo wafyatuaji hulazimika kukata miti msituni kwa ajili
ya kuweza kupata kuni za kuchomea tofari.
Valence alisema kuwa baada ya kuona uharibifu huo wa
mazingira ukiwa unaendelea katika mji huo aliona ni vyema anunue mashine ya
kisasa ambayo itaweza kufanya kazi ya kufyatua tofari za kuchanganya mchanga na
simenti, na kuwataka vijana wanaojishughulisha na kazi hiyo wajikusanye kwa
pamoja na yeye atawasaidia kuunda kikundi ambacho kitasajiliwa kisheria na
kuweza kufanya kazi hiyo ya kuwaletea kipato.
“Ninahamasisha vijana wote hapa Mbinga waje kufanya kazi hii,
lengo waachane na kazi ya ufyatuaji tofari za udongo mabondeni kwani huchangia
kuharibu mazingira yetu, vilevile kampuni inahamasisha upandaji wa miti rafiki ya maji kwenye vyanzo vyetu vya maji”, alisema Valence.
Alisema mashine hiyo ambayo ujenzi wake umekwisha anza,
anatarajia ifikapo Mei 10 mwaka huu kazi rasmi ya ufyatuaji wa tofari hizo za
simenti (blocks) utaanza na kwamba tofari moja litakuwa linauzwa kwa shilingi
1,000.
Mkurugenzi huyo wa Ovans Construction Limited aliongeza kuwa,
kampuni hiyo pia imeweza kusaidia vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani
Mbinga kuanzisha mradi wa ushonaji nguo na husimamia mikopo benki ya kikundi
cha vijana, kinachofahamika kwa jina la ‘Kusile waendesha boda boda’ kilichopo
mjini hapa ili waweze kujipatia kipato na kusukuma mbele gurudumu la maendeleo
katika maisha yao.
No comments:
Post a Comment