Na Steven Augustino,
Tunduru.
WAKULIMA wanaozalisha mazao ya aina mbalimbali wilayani Tunduru
mkoa wa Ruvuma, wametakiwa kufuata maelekezo wanayopewa na wataalamu wa ugani
wa wilaya hiyo ili waweze kujiletea maendeleo katika sekta ya kilimo na
kuondokana na umaskini uliokithiri miongoni mwao, ambao umekuwa ukiwasumbua kwa
miaka mingi katika maeneo ya vijiji vyao wanavyoishi.
Mwito huo ulitolewa na mwakilishi wa Mkurugenzi mtendaji wa
Halmashauri ya wilaya ya Tunduru, Afisa kilimo wa Halmashauri hiyo Chiza Marando
wakati akizungumza na vikundi vya wakulima kutoka vijiji vya Legezamwendo,
Kidodoma, Machemba na Mkwajuni.
Aidha Marando alisema kuwa mtindo wakati wote kuwalaumu
wataalamu hao ambao umekuwa ukifanywa na wananchi wengi katika vijiji wilayani
humo, hauwezi kuwasaidia na kwamba kinachotakiwa waitikie wito na kusikiliza
maelekezo wanayopewa ili waweze kuzalisha mazao bora.
Alisema katika kuhakikisha kwamba serikali imejipanga
kuwapelekea maendeleo, Halmashauri yake kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa
tayari imeanza kuwajengea miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji katika maeneo
yao, pamoja na kuwawekea mashine ya kukoboa mpunga kwa madaraja kwa lengo la
kuongeza thamani ya mazao yao.
Marando aliyataja maeneo waliyojenga miundombinu hiyo kuwa ni
katika maeneo ya Madaba, Legezamwendo, Lelolelo, Kitanda na Misyaje wilayani
Tunduru.
Kuhusu mashine ya kukoboa mpunga kwa madaraja alisema kuwa
imefungwa katika eneo la Nakayaya Tunduru mjini, eneo ambalo kila mkulima
anaweza kufika kwa urahisi na kupata huduma husika.
Alisema hata hivyo uzoefu unaonesha kwamba soko lipo kubwa la
zao la mpunga ambao hukobolewa kwa wingi na kuwekwa kwenye daraja la kwanza
ambao hufungwa katika vifungashio maalumu, ambavyo vimethibitishwa na
shirika la Viwango Tanzania (TBS) ambapo huuzwa shilingi 3,000 kwa kila kilo
moja kwa mchele wa daraja hilo la kwanza.
Kwa mujibu wa Marando aliongeza kuwa mikakati mingine waliyojiwekea
ni pamoja na Halmashauri yake kuweka utaratibu wa wakulima hao kuuzia mazao yao
katika maeneo yaliyoainishwa, lengo ikiwa ni kuisaidia serikali kukusanya
takwimu ambazo zitaweza kusaidia kupanga mikakati thabiti ya kuwahudumia
wakulima wake kwa kutumia takwimu sahihi.
No comments:
Post a Comment