Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
IMEELEZWA kuwa, Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira katika
mji wa Mbinga mkoani Ruvuma (MBIUWASA) endapo haitajidhatiti kuboresha utoaji
wa huduma hiyo kwa viwango vinavyotakiwa, kuna uwezekano mkubwa kwa wananchi waishio
katika mji huo kuugua homa za matumbo kutokana na maji wanayotumia sasa kuwa
machafu.
Aidha mji huo hivi sasa unakabiliwa na tatizo kubwa la uhaba
wa maji, ambapo wakazi wake wakati mwingine hulazimika kuyafuata kwenye vijito
vinavyowazunguka ndani ya mji, ambapo hali hiyo imedumu kwa muda mrefu na kuwa
kero miongoni mwa jamii.
Hayo yalisemwa na Madiwani wa Halmashauri ya mji wa Mbinga,
kwenye kikao chao cha baraza la madiwani kilichoketi juzi katika ukumbi wa Chuo
cha maendeleo ya wananchi, kilichopo mjini hapa.
Walisema kuwa huduma ya maji itolewayo sasa na Mamlaka hiyo
ni hafifu haikidhi mahitaji husika, na kwamba maji yanayosambazwa ni machafu
huku yakiwa yana rangi ya vumbi jambo ambalo ni hatari kwa afya ya binadamu.
“Maji yanayotumika katika mji wetu ni machafu, tunahitaji
MBIUWASA iboreshe huduma kwani wananchi kila mwishoni mwa mwezi wanatozwa riba
kubwa na huduma yenyewe ni mbovu”, walisema.
Malalamiko hayo ya madiwani, yalifuatia baada ya kutolewa
taarifa katika kikao hicho kwamba Mamlaka hiyo ya maji safi na usafi wa
mazingira inampango wa kupandisha bei za maji, ili iweze kupata fedha za
kuboresha miundombinu yake ya kusambaza huduma hiyo muhimu kwa wananchi.
Pamoja na mambo mengine alipotakiwa kutolea ufafanuzi juu ya
hoja hizo, Meneja fundi sanifu wa Mamlaka hiyo, Athony Modest alisema kuwa hivi
sasa maji yanayozalishwa katika mji wa Mbinga ni mita za ujazo 2,100 huku
mahitaji halisi yakiwa ni mita 3640.
Modest alikiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kwamba alieleza
kuwa uzalishaji huo wa maji kuwa mdogo unasababishwa na miundombinu husika kuwa
chakavu kutokana na mji huo hivi sasa kuwa na ongezeko kubwa la watu kadiri
siku zinavyozidi kusonga mbele.
Alisema kuwa ili kuweza kukabiliana na tatizo hilo hawana
budi kuongeza bili za maji, ili waweze kupata fedha za kutosha kukarabati
miundombinu iliyopo sasa ikiwemo ufungaji wa machujio ya maji, ambayo yatafanya
kazi ya kuchuja maji yawe safi na sio kuwa machafu.
No comments:
Post a Comment