Na Steven Augustino,
Namtumbo.
KAMPUNI ya
Mantra inayotarajia kuchimba madini ya Urani, katika
eneo la mto Mkuju wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma
imetuhumiwa kwamba imekuwa haitoi ushirikiano kwa Halmashauri ya
wilaya hiyo, pale wanapoalikwa kuhudhuria mikutano ya baraza la
Madiwani wilayani humo.
Tuhuma hizo
zilitolewa na Mwenyekiti wa baraza hilo, Daniel Nyambo mbele ya Mkurugenzi
mtendaji wa halmashauri hiyo, Ally Mpenye wakati akizungumza na Madiwani hao
katika kikao cha baraza hilo kilichoketi hivi karibuni wilayani
humo.
Wakifafanua
taarifa hiyo kwa nyakati tofauti, Nyambo na Mkurugenzi wa
Halmashauri hiyo, Ally Mpenye waliwaeleza Madiwani hao kwamba kila
wanapowalika viongozi wa kampuni hiyo kwa ajili ya kuhudhuria
vikao vya baraza hilo, hawafiki jambo linalowaletea
mashaka juu ya mambo wanayotaka kuficha wakati wa utekelezaji wa mradi huo na
madhara yanayoweza kujitokeza kwa jamii.
Aidha walibainisha kuwa
mialiko wanayoitoa kwa kampuni hiyo kuhudhuria
vikao vya baraza hilo, ili waweze kutoa elimu
kuhusu madini hayo kwa Madiwani wamekuwa
hawaonekani licha ya kampuni ya Mantra, kuisaidia Halmashauri
katika baadhi ya mambo pale inapoombwa kufanya hivyo.
Kufuatia hali hiyo
Madiwani hao waliwataka Mwenyekiti na Mkurugenzi wa Halmashauri
ya wilaya ya Namtumbo, kuendelea kuuomba uongozi wa kampuni hiyo
kutoa elimu kuhusu madini hayo ili na wao wakatoe
elimu kwa wananchi wao, juu ya madhara yanayoweza kujitokeza wakati wa
utekelezaji wa mradi huo.
Katika kutaka kujiridhisha
juu ya tuhuma hizo, mwandishi wetu alikwenda katika Ofisi za
mahusiano ya jamii ya kampuni ya Mantra iliyopo mjini Namtumbo
ambapo alikutana na mlinzi wa ofisi hiyo na kuambiwa kuwa, Afisa
mahusiano huyo ambaye alimtaja kwa jina la Khadija Pallangyo ambaye
alidai kuwa siku zote hukaa Songea mjini na kwamba, hufika
ofisini hapo pindi anapokuwa na kazi ya kufanya.
Hata hivyo Afisa
mahusiano huyo Pallangyo alipotafutwa kuzungumzia malalamiko hayo
ya Madiwani, ambao walidai kuwa kutopatikana kwa maafisa hao
kumewafanya washindwe kutekeleza mipango yao ya kutoa elimu kwa umma,
kutokana na uongozi wa Mantra kutohudhuria vikao hivyo vya baraza
la Madiwani kila wanapoombwa kufanya hivyo.
No comments:
Post a Comment